Naam mpenzi msomaji wa safu hii ya nguvu ya historia, karibu katika safu hii kwa mara nyingine tena. Leo hii tutaangazia kuhusu bunduki aina ya AK 47 na pasi na shaka wengi wanajua kwamba ni bunduki, lakini ni bunduki ya aina gani?
Ilitengenezwa na nani, lini?
Mtengenezaji alisema nini kuhusu AK-47 kabla ya kifo chake?
AK-47 ni aina ya bunduki iliyogunduliwa katikati mwa karne ya ishirini katika jamhuri ya umoja wa nchi za kisovieti au kwa jina rahisi ni Urusi ya zamani.Kuna taarifa tofauti tofauti kuhusiana na bunduki hii lakini katika safu hii tutaangazia kiini yaani aina ya AK-47 iliyobuniwa na kutengenezwa nako Urusi ya zamani.
Picha ya bunduki aina ya AK-47
Herufi na namba AK-47 ni ufupisho wa majina Automat Kalashnikov mbadala wa jina Mikhail Kalashnikov ambaye ndiye mgunduzi wa bunduki hii ya AK-47. Namba 47 inasimama kuwakilisha mwaka 1947, mwaka ambao ugunduzi wa bunduki hii ya AK-47 ulifanyika.
Mikhail Kalashnikov alianza kuibuni silaha hiyo tangu mwaka 1946 lakini matatizo ya kiteknolojia na hitaji la wakati vilichelewesha lengo la kuhakikisha silaha inazinduliwa mapema na hatimaye kila mwanajeshi msovieti anamilikishwa AK-47 kwa ajili ya kulinda muungano wa kisovieti, watu wake na mipaka.
Kwa mantiki hiyo, mpaka mwaka 1956 ndipo vikosi maalumu vya kijeshi vilisambaziwa silaha aina ya AK-47 na taarifa kuhusu uimara na nguvu ya silaha hiyo, ilikuwa tishio duniani kote haswa kwa mataifa yaliyokuwa na uhasama na umoja wa kisovieti ikiwemo Marekani.
Mpaka sasa bunduki nyingi aina ya AK-47 zinatengenezwa katika mataifa mbalimbali lakini taifa la Urusi ndilo linalotengeneza kwa kiasi kikubwa na inaaminika kwamba soko kubwa la silaha hizo ni pamoja na nchi za mashariki ya kati ikiwemo Iraq. Pia magenge ya kihalifu mathalani yale ya kigaidi na yale yanayojihusisha na madawa ya kulevya katika nchi za Mexico,Trinidad na Hong Kong, yametajwa kujiingiza pia katika biashara ya silaha hiyo maalumu kwa miaka mingi.
Inakadiriwa kuwa mzunguko wa kibiashara wa AK-47 duniani ni milioni 75 mpaka milioni 100.Ikumbukwe kuwa siyo bunduki zote aina ya AK-47 hutengenezwa Urusi bali pia mataifa mengine kama vile China, Hungary, Poland na Marekani wanatengeneza.
Aina ya AK-47 zimepata kuboreshwa kila mara kutokana na ukuaji wa teknolojia kwa lengo la kukidhi matakwa ya kiulinzi na soko la silaha duniani. Mpaka sasa AK-47 imeboreshwa zaidi na hujulikana kwa jina jipya la AKM yaani 'Automat Kalashnikov Modenizirovanniy' au kwa kifupi modernized AK kama inavyoonekana hapo chini.
Naam, hiyo ndiyo AK-47 a.k.a AKM. Mikhail Kalashnikov ambaye ndiye mgunduzi wa bunduki hii alifariki dunia mnamo mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 94 na alizikwa kwa heshima kubwa za kijeshi.Lakini kabla ya kifo chake alimwandikia barua maalumu Patriarch Kirill mnamo may, 2012. Je, barua hiyo ilihusu nini? Kwanini aliituma kwa Kirill?
Itaendelea katika makala ijayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni