Kule kwetu Mwakaleli pamoja na mambo mengine kuna msemo maarufu usemao "Imbombo ngafu" fasiri yake kwa kiswahili ni "kazi ni ngumu". Msemo hautumiki hovyo wala haitarajiwi eti mnywa viroba atoke zake gengeni harafu awakute 'Abhanyambala' yaani wanaume harafu aseme, "Imbombo ngafu" pasipo kuainisha kwa lipi?
Labda siku hizi kwa ajili ya utandawazi, wenyewe husema "Abhajanga bhatusobhisye" yaani wageni wametupoteza. Enzi hizo kina Mwakagile, Mwakyoma, Mwatogile, Mwangela, Mwandenuka, Mwalugaja, Mwakilasa na Mwatukuju wakikaa chini kujadili jambo gumu harafu Malafyale (Chief) katika mazungumzo yake akasema "imbombo ngafu" basi hapo ungetabiri kuna jambo.![]() |
Prof.Mark Mwandosya |
Sasa hapo ndo kuna 'mbombo ngafu' maana maamuzi yatakayotokana na kikao hicho basi ujue haitaangaliwa sura ya mtu bali yeyote atakayetuhumiwa kwa jambo fulani lazima awajibike.
Enzi hizo, kwanza mikutano mizito ilikuwa na sifa kuu mbili. Ya kwanza ilikuwa inaanza alfajiri na mapema jogoo wa pili akiwika halafu sifa ya pili ni kwamba kina mama hawakuwa wanaruhusiwa kushiriki vikao hivyo. Siyo kwa ubaguzi wa kijinsia bali kwasababu moja tu, kina mama wana huruma mno hivyo wanaume wakifanya maamuzi magumu huenda kina mama wakaenda kinyume japokuwa jambo hili haliaminiki sana siku hizi.
Sasa hatma ya yote hayo ni kwenye maamuzi ya "Bhanyambala" kutekelezwa hivyo kama ni mtu amethibitishwa kuwa 'mbhuti' yaani mchunaji ngozi basi basi huyo atakabidhiwa kwa 'NTAGA BHUMI KUSELESI' yaani anakabidhiwa kwa kamanda anayeshughulika na kuwatupa watu hai katika korongo la maajabu ambalo mtu akitupwa huko kamwe harudi.
Sasa Chama Cha Mapinduzi kinakabiliwa na tatizo na kumkosa 'NTAGA BHUMI KUSELESI' kwa maana waovu wanacheka na kutamba badala ya kulia na kutokwa makamasi wakiomba radhi wasitupwe SELESI. Pamoja na mambo mengine, baadhi ya wandishi wa habari wamekuwa watu wenye huruma kwa wala rushwa, mafisadi, waroho wa madaraka, wahujumu uchumi na wenye kutumia vibaya fedha zao. Pasi na aibu unakumbana na andiko eti mtia nia wa urais amepata watu elfu 9,000, 10,000 na bila shaka wiki lijalo watataja 20,000.
![]() |
Mhe.Edward Lowassa, mtia nia ya Urais kupitia CCM |
Sawa kama anapendwa ni vema, lakini ni nani anaye wahesabu watu katika hadhara hizo?
![]() |
Mhe.Steven Wassira akinadi sera kwa wana CCM eneo la Kirumba, Mwanza. |
Nimeandika makala hii maalumu kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na wapenda demokrasia ya kweli. Mbona watu wakiwa wachache hamuandiki watu wamejitokeza kumdhamini mgombea, walikuwa wame 'relax' wala hawakanyagana.
Jambo lililopo mbele yetu ni 'Mbombo ngafu' yaani kumpata mtu atakayetuvusha kutoka kwenye umasikini penye mali na maradhi penye kinga ili tusonge mbele. Kuna kitu kinaitwa 'Social Responsibility Theory', ni lazima vyombo vya habari viwajibike kuwajuza wananchi ukweli na umuhimu wa kinachoendelea. Na siyo tu kuwajibika bali pia kuwaongoza katika maamuzi sahihi.
Si lazima wala hakuna dalili za moja kwa moja kwamba Rais ajaye atatoka CCM, lakini jambo la msingi ni kwamba vyombo vya habari visaidie kukuza demokrasia na siyo kuendekeza domokrasia. Vyombo vya habari viwajuze wananchi sera za wagombea, maono yao, umahiri na ubunifu wa kiuongozi.
Tanzania imara ni matokea ya ukweli, uwazi na uwajibikaji wa kila mmoja. Tusiwatoe wananchi kwenye hoja na kuwapeleka kwenye vioja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni