Hatua ya awali pale inapogundulika dhahabu ni kusafisha mazingira, hivyo kwa kuwa hapo unapoona palikuwa ni eneo la msitu basi kilichobaki ni kuni.
Wanyama hawa huishi kwa amani panapo uoto wa asili lakini kwa kuangalia ile picha ya kwanza utagundua kwamba kizazi kijacho kitawafahamu wanyama hawa kwa kutembelea makumbusho tu.
Bila shaka umejionea mwenyewe kuhusu kule tunakoelekea hivyo endelea kunifuatilia.
Ukitazama rangi ya maji hayo hapo juu utagundua kwamba si salama wala haifai kwa binadamu kunywa, kunawa au hata kutembea peku peku kwa maana maji hayo yamechanganyikana na kemikali aina ya zebaki inayodhuru ngozi na seli hai zake. Lakini maji hayo yametoka wapi?
Najua una hamu ya kutaka kujua nakupeleka wapi lakini usiwe na haraka, kwenye picha hii utaona binadamu na wanyama wanatumia maji hayo hayo yenye kemikali huku wengine wakiyatumia hata kwa kupikia chakula.
Eneo hili ni maarufu kama sehemu ya kuoshea dhahabu na wachimbaji wadogo hulitumia eneo hili katika moja ya hatua ya kukamilisha mchakato wa kutengeneza dhahabu. Maji yanayotoka hapo hayana mkondo maalumu licha ya kujaa sumu hivyo hutiririka kwenye hicho kimto ambacho watu huyatumia maji yake kwa kupikia, kuoga na kunywesha mifugo.
Wakati kukiwa na kelele nyingi kuhusu kupiga vita ajira kwa watoto na kuhakikisha mtoto wa kike anasoma, hali sivyo kwa watu masikini mkoani Geita. Mama huyo anaponda mawe ya dhahabu sambamba na mwanae katika harakati za kujipatia mkate wa kila siku. Pahala pengine kuna watoto wadogo kuzidi huyo mtoto wa kike. Wachimbaji wadogo hawana mitaji hivyo hawana mashine za kusaga mawe badala yake kazi hiyo hufanywa na binadamu.
Kina mama wakimaliza kupondaponda mawe, zamu inahamia kwa vijana hawa ambao ni wachenjuaji wa dhahabu. Wanaosha kisha mchakato mwningine utaendelea. Hapa ni hela kwanza, afya na usalama vitafuata maana hawana namna.
Usidhani hapo wanaume wazima wanaota moto lahasha, wanachoma dhahabu ikiwa ni moja kati ya maandalizi kabla ya kuiuza kwa kudalaliwa tena kwa bei anayopanga mnunuaji. Ndiyo, sasa kama utagoma kuwauzia si ajabu ukaundiwa genge la watu wakakuvamia na kukuua kisha wakaondoka na mali.
Shughuli ya uchimbaji dhahabu imekuwa ngumu, hakuna maeneo maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Kijana huyu akiliwakilisha kundi jingine kubwa la vijana wameamua kujiingiza kwenye shughuli nyingine. Yeye mwenyewe amesema, "hatuwezi kuiba, siku kwenye magwangala kuna 'MAFIDI', wakikukamata lazima wakuache kilema. Tumeamua kufanya shughuli ya uchomaji mkaa. Maliasili wakija tunakimbizana nao hivyo hivyo. Hakuna utajiri humu kwenye mikaa lakini hatuna namna maana dhahabu ya Geita sasa ina wenyewe".
Pamoja na mambo mengine mengi, hakuna matumaini ya wananchi kunufaika moja kwa moja na rasilimali zao. Nisikuchoshe sana, makala ijayo itazungumzia athari ya zebaki kwa afya ya binadamu wakiwemo watoto wadogo kama hawa hapa.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni