Lebo

Alhamisi, 11 Juni 2015

Zijue siri kuu mbili kuhusu namna ya kumchagua mwenzi wa maisha


Miongoni mwa stori maarufu zilizopata kusimuliwa sana kuhusiana na masuala ya mahusiano katika muktadha wa mapenzi na ndoa basi ni ile stori inayowahusu wasomi maarufu na wanafalsafa mashuhuri  wa Ugiriki ya kale ambao mawazo yao yanaishi mpaka sasa, mmoja akiwa mkubwa (Socrates) na mwingine akiwa mdogo (Plato). Kwa lugha rahisi, twaweza sema mahusiano ya watu hawa wawili yalikuwa ni ya mwalimu na mwanafunzi.

Stori kuhusiana na watu hawa haswa katika muktadha wa mapenzi na ndoa zimesimuliwa sana katika vitabu mbalimbali vya uchambuzi wa falsafa na hata katika mitandao ya kijamii na blog maarufu duniani ikiwemo ile ya MOON POINTER inayopendelewa zaidi na waumini wa dhehebu la buddha. Wiki iliyopita niligusia kuhusu dillema katika kufanya maamuzi ya kuoa au kuolewa haswa pale ambapo mhusika anakuwa na mpenzi zaidi ya mmoja. Nini kifanyike basi ili kuyafikia maamuzi sahihi? Fuatilia stori hii kwa makini kisha akili za kuambiwa, utachanganya na zako.
                                                                         
Sanamu ya Socrates









                                 
Siku moja Plato alimhoji mwalimu wake ambaye ni Socrates, "Mapenzi ni nini? na nitayapataje mapenzi?"
Mwalimu wake alimjibu, "Kuna shamba kubwa la ngano mbele yako,tafadhari songa mbele wala usigeuke nyuma. Tazama mche bora zaidi wa ngano iliyochanua, chuma harafu ulete. Kumbuka ni mche mmoja tu ambao unaamini ni bora zaidi kuliko miche mingine yote shambani hapo. Ukirudi nitakuambia maana ya mapenzi".

Basi, Plato alifuata maelekezo ya mwalimu wake kuelekea shambani. Alitazama kushoto na kulia, nyuma na mbele huku akichunguza kwa umakini mkubwa miche mbalimbali iliyokuwa shambani. Plato aliendelea kusonga mbele, akitazama mbele akawa anaona kama miche mizuri ipo kule mbele siyo pale alipo na akisonga mbele pale alikuwa akiona kama mche aliouacha nyuma ni bora zaidi kuliko pale alipo.

 Plato alijipa moyo akijisemea moyoni, "bila shaka mbele kuna miche bora zaidi, ngoja nizidi kusonga". Plato aliendelea na zoezi, uzuri wa miche shambani pale ulimchanganya Plato mwisho wa siku akajikuta yupo mwishoni pasipo kuchuma mche wowote ule. Kwa kuwa Plato alikuwa anamheshimu sana Mwalimu wake hakutaka kumdanganya, alikumbuka usemi ule alioagizwa kwamba endapo atafika mwisho katu asirudi nyuma hivyo akate kona kurudi kwa Socrate.
Sanamu ya Plato
Asijue la kufanya, Plato alirudi kwa mwalimu wake huku akiwa amenyong'onyea pasi na kuwa na kitu mkononi. Socrate alipomwona Plato alimuuliza, "mbona umerudi mikono mitupu hali shamba lina miche mingi mizuri, yenye afya na mvuto"?
Kwa unyonge Plato alijibu, "tazama, kila nilipotaka kuchuma mche bora niliacha haswa pale nilipoinua macho na kuona mbele kwani macho yangu yaliniambia mbele kuna mche bora zaidi, mwisho wa siku nikajikuta nimefika mwisho pasi na kuchuma kitu na nilipokumbuka amri yako ya kutokurudi nyuma basi niliamua nije nikutaarifu kuwa nimeshindwa kuchagua mche bora nikiamini kwamba bado utaniambia maana ya mapenzi"

Socrate alimtazama mwanafunzi wake kwa jicho la huruma kisha akamwambia, "Plato, hayo ndiyo mapenzi".
Jibu lile lilikuwa msamiati mzito kwa Plato, hakuelewa mantiki ya jibu lile. Alijiuliza ikiwa mapenzi ni kukosa kuchagua, ni kuwa mzembe kutokana na tamaa ya kupata kitu bora zaidi ya kinachowezekana kukipata kwa wakati huo? Pia, Plato alijipa moyo kwamba pengine Mwalimu Socrate alimjibu vile kutokana na hasira hivyo kuna siku atampa maana halisi tena kwa ufafanuzi mwanana.
Basi Plato akakuna kichwa kisha akamuuliza Socrate, "Mwalimu, nini maana ya ndoa?"
Socrate alimtazama tena Plato kisha akamwambia, "nenda katika lile pori la jirani, ingia katika msitu ule ambao miti yake ni mizuri, imara na hata matunda yatokanayo na miti hiyo ni bora kwa hatma ya ulimwengu. Tazama mti uliobora zaidi kisha ukate na ulete hapa"

Picha ya miti yenye mvuto, ilipigwa na kuhifadhiwa mtandaoni na YEIN
 Pasipo kufanya ajizi Plato aliingia ndani ya nyumba kisha alichukua shoka na kukimbia kuelekea porini. Alipofika aliona miti mingi yenye maua na matunda ikiwa na mvuto wa pekee, alipiga hatua ya kwanza, ya pili, ya tatu aliona mti alielekea kushoto na kuanza kukata mti pasipo kujiuliza maswali mengi ikiwa mbele yake kuna miti mingine mizuri zaidi.
Ndani ya dakika 20, Plato alirudi nyumbani huku akiwa na mti begani kisha alimwambia mwalimu wake, "Nimekwenda na nimekata mti huu hapa, sikutaka ajizi hivyo nilipofika tu nikauchagua huu wala sijafika mwisho".
Socrate alicheka kisha alimwambia, "hiyo ndiyo maana halisi ya ndoa". Plato alikaa chini kisha akapumzika huku akitafakari usemi. Najua, mpenzi msomaji nawe unatafakari kitu lakini kikubwa zaidi nikukumbushe tu ule usemi wa wahenga usemao mtaka vyote kwa pupa hukosa vyote. Ukitaka kuoa usichague wala kulinganisha sana kiasi cha kukosa kufanya maamuzi bora tena kwa wakati sahihi vivyo hivy kwa uanayetaka kuolewa.
Kwa maswali, maoni na ushauri basi usiache kuwasiliana nami. Labda tu nikutamatishie stori ya mwalimu Socrate na mwanafunzi Plato. Majumuisho ya stori nzima aliyatoa mwalimu socrate akisema, " Kwa namna yoyote ile, mwanaume inabidi afunge ndoa ili kama atampata mke mwema basi ataishi maisha ya furaha lakini kama atakosa basi atageuka na kuwa mwanafalsafa". 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni