Plato, mwanafalsafa maarufu wa Ugiriki ya kale mpaka siku hizi aliwahi kushuhudia kwamba alikuwa anamshukuru Mungu kwa mambo makubwa mawili ambayo yeye alipenda kuita upendeleo maalumu. Plato alimshukuru Mungu kwa kuwa alimuumba kuwa Mwanaume na si mwanamke. Jambo la pili, Plato alimshukuru Mungu kwa kuwa yeye Plato alizaliwa kama mtu huru na siyo mtumwa. Kwa kuthibitisha uimara wa shukrani zake, Plato aliamua kuishi Kapela maisha yake yote yaani hakuoa.
![]() |
Sanamu ya Plato |
Mwanafalsafa mwingine maarufu ambaye pia ni jamaa wa karibu wa Plato almaarufu Socrates, yeye alifunga ndoa. Pengine alitaka kuuthibitishia ulimwengu kwamba mwanaume aweza kubaki mwenye hekima licha ya kuishi na mwanamke. Socrate yeye aliamini kwamba hekima ya mwanaume haiwezi kudhoofishwa na uwepo wa mwanamke karibu.
Nabii maarufu katika bara Asia aliyejulikana kama Gautama ambaye baadaye alikuja kujulikana kama Buddha, yeye aliasi ndoa na kisha aliamua kuishi mwenyewe.Gautama alijulikana sana kwa nguvu za kiroho na alipata wafuasi wengi duniani kote.
Kwa maelfu ya miaka, wayahudi wanaume walisali wakisema, "Utukuzwe Mungu Baba na Bwana, kwa kuwa haukuniumba mimi kuwa mwanamke".
Bwana Yesu hakuoa, alitoa miongozo michache kuhusiana na mambo ya mapenzi, zinaa na upendo katika familia. Alikula na kunywa pamoja na wazinifu huku akihubiri umuhimu wa kusamehe na kuishi kwa upendo katika familia.
Mtakatifu Paulo,aliamuru kwamba ilikuwa vema wanaume wasioe lakini alisisitiza kwamba ndoa ingependelewa zaidi kuliko zinaa. Kwa mawazo yake binafsi, Mt.Paulo hakupendelea kuwafundisha watu kuhusu mamlaka ya wanawake. Alionya kwamba ni vema wanawake wakajishusha na pindi wapatapo mafundisho katika nyumba za ibada basi ni vema wakawa na unyenyekevu mkubwa.
![]() |
Picha ya Mtakatifu Paulo |
Mtume Mohammed alifunga ndoa mara 14, pia alielekeza katika Koran kwamba wanaume wawaadhibu wake zao pindi wafanyapo makosa ili kulinda heshima ya mwanaume na kuimarisha nidhamu katika familia.
Mtakatifu Augustino, hakuona tofauti kati ya ndoa na zinaa kwani yote ni makosa. Watoto wanazaliwa katika mazingira ya dhambi hivyo ni lazima wabatizwe na kutakaswa baada ya sala na toba. Na huu ndiyo mwanzo wa dhana ya utakaso au 'Doctrine Celibacy'. Hata mwasisi wa taifa la India ndugu Mahatma Gandhi alimshukuru sana Mungu pale uzee ulipomkaribia kwa kasi. Aliamini kwamba aibu ya miaka mingi ya kufiwa na mwanae ilitokana na walakini katika muktadha wa zinaa katika ndoa.
Yote tisa, kumi ni kwamba; kipi ni kweli kuhusu ndoa, mapenzi na wanawake?
Waweza kuwa na wapenzi wa kike watano na wote unawapenda, ukiwaza kumuoa mmoja unahisi hakufai sana ukilinganisha na wale uliowahi kuwa nao na zaidi unayo matumaini makubwa kwamba utakutana na mzuri zaidi. Umri unakwenda, uzee unakunyemelea na hofu juu ya ndoa inautesa moyo wako.
Ukisoma historia ya watu maarufu kuhusu ndoa, unashindwa kuamua yupi umpe nafasi ya kuishi nae milele. Vivyo hivyo kwa kina dada.
Sasa usipate tabu, katika makala ijayo kuhusu mapenzi utapata kujua kuhusu mbinu kuu mbili za kumchagua mpenzi na hatimaye mwenzi wa ndoa.
Kwa maswali, maoni na ushauri tafadhari usiache kuwasiliana nami.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni