Lebo

Alhamisi, 11 Juni 2015

Hekaheka za kutafuta wadhamini, Membe aibukia Mbeya

Katika kile tunachoweza kuita hekaheka za kusaka Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Mhe. Bernard Membe amezua gumzo jijini Mbeya kutokana na umati mkubwa wa watu kujitokeza kumpokea na kutaka kumdhamini. Waziri Membe ambaye pia amewahi kuwa Kachero wa usalama wa taifa kwa miaka 15 mfululizo anaelezwa mwanadiplomasia mahiri na mwadilifu ambaye hana skendo yoyote ya rushwa na ufisadi.

Pamoja na hayo, wanamageuzi wenye msimamo mkali wanamuelezea Mhe. Membe kama aina ile ile ya matunda ya CCM hivyo hawezi kubadili mfumo na ombwe la uongozi ndani ya CCM ambapo pia ndicho chama dola. Mhe.Bernard Membe, pamoja na watu wengine, pia anapigiwa chapuo na Mzee George Kahama, aliyekuwa rafiki mkubwa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kitendo cha Mzee mwingine ambaye ni Kingunge Ngombale Mwilu kuzamia kambi ya mtia nia mwingine ndani ya CCM ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani aliyejiuzulu kwa kashfa ya ufisadi wa RICHMOND, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa ni ishara ya mnyukano mkali ndani ya CCM katika harakati za kumtafuta mgombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho kikongwe nchini.
 

                                                                         
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Bernard Membe akiwapungia mkono wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na wananchi waliofika kumpokea nje ya Ofisi ya CCM Mkoa wa Mbeya jana June 10, 2015 baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kutafuta wadhamini watakaotia saini fomu zake za kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya chama hicho.


Mhe.Bernard Membe akiwahutubia wananchi waliofika kumsikiliza jijini mbeya.
Wadadisi wa mambo ya kisiasa nchini wanasema mchuano bado hautabiriki kutokana na wingi wa watia nia sambamba na umahiri wao japokuwa wengi wanatajwa kama wasindikizaji. Lakini pia kitendo cha watia nia kupitia CCM kuukacha mdahalo ulioandaliwa na CEO Round Table ni kitendo kinachoelezwa kuwa ni udhaifu wa baadhi ya wagombea ambao aidha si waadilifu au hawajui kujenga hoja zenye ushawishi mbele ya umma hivyo wanaogopa kuaibika.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni