![]() |
Mhe.Steven Wassira akinadi sera Kirumba, Mwanza |
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhe. Steven Wassira amegeuka na kuwa mchekeshaji katika harakati za kuusaka Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hii ni baada ya kutoa kauli yenye utata na ambayo imetafsiriwa kuwa ni kichekesho miongoni mwa wananchi waliofika kumsikiliza katika harakati zake za kuelekea ikulu.
Pamoja na mambo mengine ya msingi, Mhe.Wassira amesema anawashangaa wagombea wenzake kwa kutoa fedha wakilenga kununua uongozi wakati uongozi siyo biashara.
Wasira alitoa kauli hiyo jana wakati akiwashukuru wanachama wa CCM
waliojitokeza kumdhamini katika Uwanja wa CCM Kirumba, kama sehemu ya
utaratibu wa chama hicho kuelekea mchakato wa kumpata mgombea urais
katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
“Jamani wakati wa kujaza watu kwenye viwanja bado haujafika, mikutano
ya hadhara bado. Kwa hiyo si kwamba hatuwezi kujaza watu, tukitaka
tunaweza, lakini wakati bado, utafika tutajaza watu."
“CCM na taifa kwa sasa vipo katika mazingira magumu kisiasa, rushwa
sasa inainyemelea kwa kasi kubwa siasa, hii ni hatari sana, kamwe tusije
kubali nchi yetu kuwekwa rehani na kundi la mafisadi.
“Mtu ambaye anataka kuiweka rehani nchi kamwe hawezi kuwa na hoja, ndio
sababu mmeanza kuona watu wanaishiwa hoja. Mtanzania yoyote yule
anayetumia mabilioni kununua nchi mwisho wa siku ataiuza tu,” alisema
Wasira huku wadhamini wake wakishangilia.
Wasira alisema tatizo la rushwa katika siasa ni kubwa kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa wanaweza kuinunua CCM.
“Hivi nani kakutuma kuinunua CCM? Unainunua kwa niaba ya nani. Nchi
yetu haipo sokoni, na wala hatujawahi kutangaza tenda ya kuuza nchi,
sasa mabilioni kwenye siasa ya kazi gani?” alihoji.
Aliwasihi Watanzania kuwa makini kwa sababu kuna kila dalili nchi inapelekwa sokoni na watu wachache wasio itakia mema.
Kada huyo mkongwe wa CCM aliwataka Watanzania kujiuliza na kutafakari
ni wapi mabilioni yanayotumika yanatoka, na kuongeza kuwa wanaotoa fedha
hizo uwezo wao kifedha hauonekani katika kulipa kodi.
Aliwataka wananchi kukataa kugeuzwa kuku wa kienyeji, ambapo alitoa
mfano wa mtu anayetaka kuwakusanya kuku huwakusanya kwa kuwarushia mtama
au pumba, nao hukimbilia kula bila hata kutaza nyuma au kufikiri.
“Kuna wenzetu ambao kwa malengo yao maovu wameamua kuwageuza wananchi
na kuwafanya kuku wa kienyeji, wanakuja na fedha zao na wanazitumia
kuwakusanya kwenye viwanja, wananchi kataeni, vinginevyo majuto ni
mjukuu,” alisema.
Tayari Wasira amekwishapata wadhamini katika mikoa 20, ikiwamo sita ya
Tanzania Visiwani na jana alidhaminiwa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga
na Geita.
Kwa upande mwingine wagombea wengine ambao ni Januari Makamba na Edward Ngoyai Lowassa wametajwa kuwa lulu mikoani.
![]() | ||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
Mhe.January Makamba akizungumza na wana CCM mkoani Iringa |
Mhe. January Makamba ameripotiwa kujizolea wadhamini 600 mkoani Iringa ambapo mchakato maalumu ilibidi ufanyike ili kuwapata wawakilishi wachache.
Kwa upande wa Mhe. Lowassa ameripotiwa kung'ang'aniwa na wananchi mjini Shinyanga wote wakitaka kumuona.
![]() | ||
Mhe.Edward Lowassa akisalimiana na wananchi mjini Shinyanga. |
Pamoja na mambo mengine, shughuli iliyonogesha safari ya Lowassa mjini Shinyanga ni pamoja na kitendo cha Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Steven Maselle kutangaza kumuunga mkono Mhe.Lowassa.
Duru za siasa kutoka vyanzo vya ndani ya CCM vinaeleza kuwa Mhe.Edward Lowassa yumo katika matazamio ya jina lake kukatwa mapema katika kinyang'anyiro hiki kutokana na kile kinachoelezwa kuwa matumizi mabaya ya fedha zake. Lakini hili laweza kuwa tetesi tu, maana siasa za CCM hujielekeza zaidi kwa mgombea mwenye kutabirika katika muktadha wa ushindi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni