![]() |
Mhe.Joseph Mbilinyi akiwa na mzazi mwenza Faiza Ally sambamba na mtoto wao kabla ya migogoro kuanza |
Jana ilikuwa siku ya aina yake kwa msanii Faiza Ally na mzazi mwenzake, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’. Wakati Faiza akimwaga chozi katika chumba cha habari katika gazeti la Mwananchi alipofika kutoa ujumbe wa kuomba radhi kutokana na vazi la kitenge lenye kambakamba alilovaa siku ya Tamasha la Tuzo za Muziki za Kilimanjaro, Sugu alimwaga chozi bungeni Dodoma alipowataka wabunge wasijadili mambo yake ya faragha.

Faiza akiwa amevalia baibui na kufunika kichwa kwa
hijabu, alieleza kwamba anajutia kutokana na kuvaa vazi lililoonyesha
sehemu kubwa ya makalio yake alilodhani ulikuwa ubunifu. Mrejesho
alioupata kuzomewa na jamii na picha zake kusambazwa kwenye mitandao ya
kijamii aligundua amefanya kosa.
Pigo la pili, ambalo limemjeruhi vibaya moyoni ni
mzazi mwenzake, Sugu kufungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo ya Sinza
iliyompa haki ya kukaa na mtoto wao kwa madai mama yake kukosa maadili.
Hivi sasa Faiza anaona dunia imemwelemea anajuta
na ameapa kutorudia tena kosa hilo. “Siwezi kurudia kosa, nitakuwa
makini zaidi katika mavazi yangu,” alisema msanii huyo, huku akitokwa
machozi alipozungumza jana na mwandishi wa habari hizi kwenye ofisi za
gazeti hili zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam.
Mwanadada huyo aliyewahi kuwa mrembo wa Tabata
namba tatu katika mashindano ya mwaka 2005 na ambaye hujishughulisha na
utayarishaji filamu, aliomba radhi kwa jamii kutokana na utovu wa
maadili aliouonyesha siku ya tuzo hizo na bado anaomba wamsamehe.
“Wasanii wengi ni wabunifu na hufanya mambo kwa
nia ya kufurahisha mashabiki kama ambavyo amekuwa akifanya Joti kuvaa
nguo za kike na kupaka rangi ya mdomo, hivyo mavazi yangu yalikuwa na
lengo la kutoka tofauti mbele za mashabiki wangu, lakini kwa
yaliyonikuta hasa kwenye vazi la Kili niliomba msamaha kwa jamii na bado
naomba wanisamehe,” alisema Faiza.
Hata hivyo, hilo la mzazi mwenzake kupewa haki ya
kisheria na mahakama kumchukua mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili na
miezi minane, kwa madai kadhaa ikiwamo ya uvaaji usiokuwa na staha, ni
jeraha kubwa lililomfanya apite kwenye vyombo vya habari kupaza sauti ya
kuomba radhi.
Sakata hilo pia limetua bungeni na baadhi ya
wabunge wanawake walimlaumu Sugu wakidai kampora mtoto mzazi mwenzake
kwa vile ni mnyonge, lakini jana mbunge huyo, aliyewahi kutamba nchini
na muziki wa Hip Hop alitoa ufafanuzi wa kina na kuwataka wabunge
wasiingilie maisha yake ya faragha.
“Wabunge tuliomo humu ndani, baadhi wametumia
madaraka yao vibaya katika kuwanyanyasa wanawake. Ninasema haya kwa
sababu nina ushahidi. Tuna mbunge mwenzetu amemnyanyasa mwanamke
mwenzetu, ameenda kutumia siku moja mahakamani kumnyang’anya mtoto wa
miaka miwili, kitu ambacho kwa kweli wanaume waangalie namna ya kuwaenzi
na kuwaheshimu wanawake hasa katika suala la kulea watoto. Ni mbunge
kutoka Chadema kama Chadema wanathamini utu wa mwanamke wangemshauri
mbunge mwenzao,” alisema juzi mbunge wa viti maalumu (CCM), Martha
Mlata.
Hata hivyo, jana Sugu alijibu kwa uzito akieleza
taratibu alizotumia kufungua kesi mahakamani, uamuzi ulivyotolewa na
namna alivyomwacha kwanza mtoto kwa mama yake yafanyike majadiliano ya
kifamilia.
“Kwa taarifa tu pamoja na mahakama kunipa haki,
mtoto bado yuko kwa mama yake kwa sababu mimi ni mstaarabu, nimetoa
nafasi ili majadiliano ya kifamilia yafanyike. Naomba mjadala huu
usiendelee zaidi ya hapa,” alisema Sugu ambaye alionekana akifuta
machozi akisikitishwa suala hilo kuzua mjadala bungeni.
SOURCE; mwananchi newspaper
SOURCE; mwananchi newspaper
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni