Lebo

Jumapili, 5 Julai 2015

MAKALA MAALUMU:CCM NA GOLI LA MKONO UCHAGUZI MKUU 2015, USALAMA WA NCHI MTEGONI

Vijana wa Green Guard ya CCM wakifanya show off

Kama kuna sifa ambayo binadamu anaweza kujitofautisha na viumbe hai hai vingine mathalani miti wanyama wa kufugwa basi ni ile sifa yake ya kutembea au kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Na mimi katika kutembea kwangu mikoa mbalimbali hapa Tanganyika, siyo tu kwamba nimetekeleza kwa vitendo msemo usemao tembea uone, bali pia nimejionea namna ambavyo baadhi ya shule za msingi wilayani Mufindi hazina madawati ya kutosha wakati kila siku mbao zinavunwa katika msitu wa Sao Hill.

Pia, nimejionea namna ambavyo baadhi ya vijana jijini Dar es salaam wamepoteza dira na matumaini ya kufanikiwa katika maisha. Wengine ni wahitimu wa vyuo vikuu, shule za sekondari na zaidi ni kwamba wana vipaji tofauti ambavyo kwa namna moja ua nyingine vipaji vyao vingetumika vema basi taifa lingepiga hatua kiuchumi, kisiasa na kijamii. Badala yake vijana hawa wamejiingiza katika urahibu wa madawa ya kulevya na hatimaye 'KUKATA RINGI' na pengine wameambulia kukamatwa na kusweka rupango kila mara hali inajulikana fika kwamba vijana hao hawana uwezo wa kwenda Pakistan, Hong Kong, Trinidad au Malaysia kwenda kufata madawa ya kulevya, je wahusika wakuu wa shughuli hii hawafahamiki daima?

Tuyaache hayo, katika kutembea kwangu nimejionea namna ambavyo mji wa Geita umejaa siasa za maji taka na ukiritimba uliozidi, mpaka leo mji huu hauna maji safi na salama achilia mbali japo kiwanda cha kutengeneza jojo ili vijana wapate ajira baada ya maeneo waliyokuwa wakichimba dhahabu kupewa wawekezaji. Sina lawama sana kwa vijana wengi waliojiingiza katika biashara ya mkaa na kufilisi miti karibia yote katika msitu wa Kukuluma. Potelea mbali mabadiliko ya hali ya hewa maana hakuna namna, ndivyo wasemavyo vijana wengi.


Yote tisa, kumi ni kuhusu jambo moja ambalo limenisumbua kwa miaka karibia 24 na leo nimeamua niliweke bayana. Kuna mtu mmoja huwa ninakutana nae kila pahala ninapotembelea na sielewi kama huwa ananifuatilia kwa siri au basi tu tunakutana kwa bahati mbaya kama vile ambavyo eneo la vwawa lilikutana na kimondo hapa duniani kule wilayani Mbozi.
Awali, nilikutana na jamaa huyu eneo la bonde la Mwakaleli kule mkoani Mbeya. Cha ajabu huyu ni mtu maarufu na karibia koo zote wanamjua huyu jamaa kuanzia kwa Mwasandube, Mwalugaja, Mwambope, Mwangela, Mwandosya, Mwakatuma, Mwakilasa, Mwangosi na hata ukoo wa Mwasanguti wanamjua vema mtu huyu anayependa kunifuatilia. Sijui kama amejiajiri au ameajiriwa kunifuatilia ila niseme ukweli tu kwamba nina mashaka makubwa kuhusu mtu huyu haswa kwa huu mwaka wa uchaguzi.
Image result for pictures of Nape Nnauye
Mhe.Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM

Kwa kule Mwakaleli nakumbuka walikuwa wanamuita "Silule". Hili ni jina la kejeli likimaanisha mtu anayejifanya anajua kila kitu, hashauriki na hata akishauriwa leo basi kesho atarudia makosa yale yale. Pamoja na sifa nyingi anazojipamba nazo Silule, sifa yake kubwa ni kudharau wengine na kupuuza yajayo hivyo ana kasumba ya kuropoka pasipo kupima athari ya maneno yake siku za mbeleni.
Sasa kasheshe ni pale Silule anapokabidhiwa dhamana ya uongozi au cheo, hakika ataapa kutawala milele tena kwa hila zote ili mradi tu anawapa wakubwa zake wanachokipenda pasi na kujali haja ya anaowaongoza au kuwatumikia. Huyo ndiye Silule. Baada ya kuivumilia kwa kipindi kirefu tabia yake, nilifanya maamuzi magumu kuliko yale maamuzi magumu ya fisadi anayejiuzulu bila kushitakiwa. Na laiti kama ningekuwa nazungumza na vijana wenzangu wa pale Isanu, Tunduma basi ningesema..."Nakhatele ni nene sya silule" yaani nilichoka na maudhi ya Silule.

Niliamua kusafiri kwenda mbali kabisa na mkoa wa Mbeya nikiamini kwamba kamwe Silule hatanifuata huko lakini kumbe nilikuwa naota ndoto za Alinacha. Siku moja nikiwa uhamishoni huko Bukoba mjini, gafla nikamwona Silule ambaye kama si yule niliyemwacha Mbeya miaka kadhaa iliyopita basi wanafanana mwili, sauti, nguo na hata akili tena kwa asilimia mia moja. Ilikuwa mwezi uliopita, Silule alivalia shati kama kombati hivi lenye rangi ya kijani. Nilimuuliza Mzee Byera kuhusu vazi lile, alinijibu kwamba huenda mhusika ameamua kuvaa vile ili aendane na rangi ya migomba yaani ule ukijani. Wala sikumwambia kama ninamfahamu mtu yule.

Kivumbi kilikuwa siku ya kesho yake ambapo Silule alikuwa mmoja kati ya wazungumzaji katika mkutano wa hadhara, unaweza ukatabiri alisema nini?
Hapana, najua wewe si mtabiri wa hali ya hewa ila Silule alisema eti waliotuhumiwa kujiandikisha mara mbili katika daftari la kudumu la wapiga kura huko Njombe na maeneo mengine ya nchi ni wale wanachama wa vyama vya upinzani sana sana wana-UKAWA. Usiniulize kama alijuaje maana jibu sina maana hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuthibitisha shutuma hizo, kibaya zaidi ni pale ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Damian Lubuva alipokataa kuwa taarifa hizo ni za kweli na zimetolewa na ofisi yake. Jaji Lubuva alisema ni kweli kuna watu wamekamatwa kwa kosa hilo lakini haijulikani ni wa chama gani.

Tuliporudi nyumbani Mzee Byera alikuwa amenuna mno, nikamhoja kulikoni? Alinijibu, "Yule Kangambeyo nilidhani ataongea mambo ya maana kumbe shutuma za kitoto na propaganda za kizamani loh". Hapo sikuuliza swali lingine maana niling'amua kiutu uzima kwamba kumbe yule Silule wa Unyakyusani akiwa huku Uhayani anaitwa Kangambeyo. Binafsi nilikereka sana na siku hiyo hiyo nikafungasha virago kwenda Mwanza ili nisije kumwona tena wala kusikia tena maneno ya Kangambeyo. 
Na ili azma yangu itimie sikutaka kukaa katikati ya jiji la Mwanza, nikaenda mpaka kijiji cha Igombe kilichopakana na kambi ya jeshi ya Igombe kama kilomita mbili kutoka airport. Cha ajabu nilipofika tu Igombe ilikuwa siku ya jumatano kulikuwa na gulio, nikakutana tena na huyu jamaa. Nahisi alikuwa ananifuatilia, stori za kila kijiwe zilimhusu huyu Silule au Kangambeyo ila niligundua kwamba kumbe alipokuwa huko Usukumani anaitwa Mushilimu ila ni mtu yule yule mmoja. 

Kimsingi nina maelezo ya kujaza kurasa nyingi za kitabu kumhusu Silule au Kangambeyo au Mushilimu ila sasa naomba maelezo yake yaishie hapo ili niende kwenye kiini cha makala hii.
Wiki kadhaa zilizopita, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Moses Nnauye alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema kwamba, "CCM kitashinda katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais utakaofanyika mnamo oktoba 25, 2015 hata kwa goli la mkono". Kimsingi kauli hii imewakera wananchi wengi wanaopenda demokrasia ya kweli na uchaguzi uliohuru na haki. Na ninaamini nikimpigia simu Mzee Mwatogile kule Unyakyusani atasema kauli hiyo imetolewa na Silule, nikimpigia simu Mzee Rutashobya kule Uhayani atasema mtoa kauli hiyo ni Kangambeyo na bila shaka Mzee Masanja wa Usukumani atasema mtoa kauli hiyo ni Mushilimu.

Wakati asasi za kiraia, taasisi za dini na wanaharakati wakihamasisha watu wajiandikishe ili wapate viongozi bora, makini na wasiokumbatia ufisadi, Nape Nnauye anasema kazi hiyo ni bure maana CCM watashinda kwa namna yoyote ile. Na ni kweli, nimepata kushuhudia maeneo kadhaa mabalozi wa CCM wanaenda na madaftari yenye majina ya watu katika vituo vya kujiandikisha wapiga kura. Si tu kwamba mabalozi wa CCM siyo watendaji wa tume ya taifa ya uchaguzi bali pia kuna utata kuhusu majina wanakoyatoa tena siku ya kwanza ya kujiandikisha. Binafsi niliwaona mabalozi wawili Mzee Rusheke katika kituo cha shule ya msingi Mkoani na Mzee Duwa katika kituo cha shule ya msingi Nyanza. 
Unashangaa, sisemi hilo ndilo goli la mkono la Mhe. Nape ila inaweza kuwa sehemu ya kile ambacho kwenye mpira kinaitwa 'counter attack' kuelekea goli la mkono.
Vijana wa Red Brigade wa CHADEMA wakionesha heshima zao kwa Mwenyekiti wa chama Mhe.Freeman Mbowe

Kinachonitia hofu zaidi ni mantiki ya goli la mkono, mfano wanachama wawili wa CUF wamepigwa risasi katika eneo la kujiandikisha katika eneo la Makunduchi huko Zanzibar. Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Arahma, ni kweli wahusika hawajulikani lakini itakuwaje watu wakihusianisha tukio hilo na harakati za goli la mkono?
Kwa kuwa Mwenyekiti wa CCM pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu na mara kadhaa tumeshuhudia wakuu wa mikoa na wilaya wakitoa amri kwa wanausalama haswa jeshi la polisi, je kwanini tusiwe na hofu kwamba yeyote atakayelipinga goli la mkono atapigwa au kubambikiziwa kesi? Pia, tunahoji kama wapinzani wapo tayari kufungwa goli la mkono?
Kwa nini nisiwe na hofu wakati najua kwamba maadui wa ndani na nje wanaweza kutumia njia ile ile ya goli la mkono kujipenyeza katika uwanja wa kuzua fujo, uhasama na mauaji katika taifa? Pengine, jambo linalotia simanzi ni ukimya wa Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais aliyeapa kuitumikia na kuilinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tuamini kwamba haoni hatari katika kauli iliyotolewa na katibu mwenezi wa chama chake?
Kama ndivyo basi mimi sitaki bughudha, wiki ijayo naanza safari ya kwenda mafichoni huko Garissa, Kenya kwa Mhe.Uhuru Kenyatta potelea mbali Alshaabab maana afadhali adui anayejulikana kuliko kusubiri tukio la goli la mkono litakalofungwa na Silule, Kangambeyo au Mushilimu. Refa kateuliwa na bosi wa Mushilimu hivyo haki haitakuwepo na bila haki amani haidumu.
Kwaheri ya kuonana!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni