Lebo

Ijumaa, 10 Julai 2015

Mapinduzi mengine yaandaliwa Burundi

Rais Pierre Nkurunziza
Mmoja wa viongozi katika mapinduzi yaliyozimwa nchini Burundi hivi karibuni ya kumpindua Rais Piere Nkurunziza ameiambia BBC kuwa waasi wao wamekuwa wakiwapa mafunzo polisi na askari kwa ajili ya jaribio jingine la kumwondoa rais Pierre Nkurunziza.
Akiwa uhamishoni Generali Leornard Ngenda Kumana amekanusha kuwa walisaidia na mataifa ya nje.
Wamekuwa wakimshutumu Rais Nkurunziza kuwa kusababisha vurugu kaati ya jamii ya wahutu na watutsi na kuwapa silaha wapiginaji wa vijana waoiunga mkono serikali ambao wanaonekana wengi ni kutoka jamii ya wahutu.
Zaidi ya watu laki moja wamekimbia nchi hiyo wakihofia vurugu wakati wa uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Wanaompinga wanasema hatua ya kugombea urais kwa muhula wa tatu kwa rais huyo ni kinyume cha katiba.

Alhamisi, 9 Julai 2015

Viongozi wa upinzani wakamatwa Uganda

Waziri mkuu wa zamani Uganda Amama Mbabazi
 Aliyekuwa waziri mkuu Amama Mbabazi alikamatwa na polisi akiwa mjini Jinja mwendo wa saa moja kutoka jijini Kampala, akiwa njiani kuelekea mkutano wake wa kwanza wa hadhara na wafuasi wake mjini Mbale mashariki mwa nchi.
Siku ya Jumatano Polisi nchini Uganda walitoa taarifa kusema kuwa bwana Mbabazi hana ruhusa ya kufanya mikutano yoyote ya kisiasa japo alikuwa amewataarifu.
Bwana Mbabazi ananuia kutafuta uteuzi wa chama kinachotawala NRM kuwa mgombea wake rasmi wa Urais katika uchaguzi huo Machi mwaka ujao.
null
Dr. Kizza Besigye
Kwa upande mwingine wa nchi mwansiasa mwingine wa Upinzani Kizza Besigye alikamatwa na polisi akiwa nyumbani kwake. Dr. Besigye , ambaye ni kanali mstaafu wa jeshi amewahi kuwania urais wa nchi hiyo mara tatu bila mafanikio.
Alikamatwa akiwa njiani kwenda kwenye mkutano wake wa kwanza na wafuasi wa chama chake cha Forum For Democratic Change.
Msaidizi wa Dr Besigye ameiambia BBC kuwa mwanasiasa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi karibu na nyumbani kwake. Besigye anashindania kiti hicho cha FDC na aliyekuwa kamanda wa jeshi Gen. Mugisha Muntu.
Dr. Besigye pamoja na bwana Mbabazi wote walikuwa washirika wa karibu zaidi na rais Yowei Museveni ambaye atashindana nao katik auchagzui huo.Museveni amekuwa uongozini kwa miaka thelathini.
Kwa sasa #FreeBesigye inaendelea kutajwa kwa wingi katika mitandao ya kijamii, baada ya watu kugeukia mitandao hiyo kuelezea hisia zao kuhusu kukamatwa kwa wawili hao.
SOURCE:BBC Swahili

Mwanamme mzee zaidi duniani aaga dunia

 Mwanamme mzee zaidi duniani raia wa Japan Sakari Momoi ameaga dunia mjini Tokyo akiwa na umri wa miaka 112.
Mwalimu huyo mkuu wa zamani wa shule ya upili na baba wa watoto watano, aliaga dunia kutoka na ugonjwa wa figo katika kituo kimoja cha kuwahudumia watu wazee siku ya Jumapili.
Alikuwa ametambuliwa na Guinness World Records mwezi Agosti.
Momoi alizaliwa mwaka 1903 mjini Fukushima na alikuwa mwalimu kabla ya kupanda cheo na kuwa mwalimu mkuu kwenye shule kadha nyumbani kwao.
Alikuwa na mazoea ya kusoma hasa mashairi ya Kijapan na pia alipenda kusafiri sehemu mbali mbali nchini Japan na mkewe ambaye sasa pia marehemu.
null
Alitambuliwa na Guinness World Records mwezi Agosti.
Wakati alipata cheti kutoka kwa Guinness World Records mwezi Agosti aliwaambia waandishi wa habari alitaka kuishi miaka miwili zaidi. Guinness bado haijatangaza mwanamamme mwenye umri mkubwa zaidi duniani baada ya Momoi.
Mwezi Aprili mtu mzee zaidi na mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi duniani Misao Okawa kutoka Japan aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 117 na sasa rekodi inashikiliwa na mmarekani Susannah Mushatt Jones ambaye ana umri wa miaka 116.
Mtu ambaye aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka ufaransa ambaye aliishi miaka 122 na siku 164 . Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.

Jumapili, 5 Julai 2015

ALI KIBA: NILISTAHILI KUPEWA TUZO TANO ZA KMA






ali-kiba-slider
Msanii Ali Kiba
Ali kiba ambaye alipata tuzo sita na kumshinda msanii wa kimataifa Diamond Platinum amesema kamwe hakupendelewa na kwamba ni muziki wake unaopendwa na wengi.
Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen siku ya ijumaa usiku nchini Kenya,Kiba amesema kuwa anahisi yeye ndio bora na kwamba ilikuwa haki yake kushinda tuzo hizo.
''Nahisi kwamba mimi ndio bora na nilifaa kushinda tuzo hizi.''Mashabiki wangu waliukosa mziki wangu na ndio maana walinipigia kura na ndio maana nilishinda tuzo sita kati ya saba nilizoteuliwa'',alisema.
Image result for pictures of diamond platnumz
Msanii Diamond Platnumz
Na alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na Diamond,Kiba alikana madai kwamba wawili hao hawana uhusiano mwema.
''Sina uadui wowote kati yangu na Diamond na haujakuwa''. Naweza kukuhakikishia kuwa mimi na Diamond hatujapigania kuhusu chochote''.
Hatahivyo amesema kuwa inamkera wakati watu wanapomlinganisha na mwimbaji huyo wa Mbagala.
Alisema:Mimi ni mimi na Diamond ni Diamond.

Dawa mpya ya ukimwi yakosolewa


Kwa muda mrefu wahudumu wa afya ya masuala ya ngono wamesisitiza matumizi ya mipira ya kondomu kama mbinu bora zaidi dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Lakini tabia moja hatari ya kutumia madawa ya kulevya na wapenzi wa jinsia moja inazidi kuibua wasiwasi.
kumekuwa na njia nyingi za kinga dhidi ya virusi vya ukimwi, lakini kuna dawa moja mpya - Pre-Exposure Prophylaxis (PrEP) - ambayo inaweza kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya ukimwi iwapo itatumika kabla ya kushiriki ngono.
Utafiti unaofanywa na daktari Sheena McCormack kutoka chuo kikuu cha London, unasema kwamba unapomeza dawa hiyo, inazuia maambukizi ya ukimwi kwa kuzuia ongezeko la virusi, hii ni baada ya majaribio kufanyiwa kundi moja la wapenzi wa jinsia moja, ambao wamo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi
Shirika la afya duniani limetambua kwamba dawa hiyo ya tembe inaweza kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya wakosoaji wanasema kuwa dawa ya aina hii inahamasisha watu wengi kushiriki ngono bila kutumia mipira ya kondomu
Hata hivyo matumizi ya dawa hii haizuii maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kisonono na kaswende, je, kukubalika kwa matumizi ya dawa hii duniani kunamaanisha ongezeko la magonjwa ya zinaa.
Source: BBC Swahili

MAKALA MAALUMU:CCM NA GOLI LA MKONO UCHAGUZI MKUU 2015, USALAMA WA NCHI MTEGONI

Vijana wa Green Guard ya CCM wakifanya show off

Kama kuna sifa ambayo binadamu anaweza kujitofautisha na viumbe hai hai vingine mathalani miti wanyama wa kufugwa basi ni ile sifa yake ya kutembea au kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Na mimi katika kutembea kwangu mikoa mbalimbali hapa Tanganyika, siyo tu kwamba nimetekeleza kwa vitendo msemo usemao tembea uone, bali pia nimejionea namna ambavyo baadhi ya shule za msingi wilayani Mufindi hazina madawati ya kutosha wakati kila siku mbao zinavunwa katika msitu wa Sao Hill.

Pia, nimejionea namna ambavyo baadhi ya vijana jijini Dar es salaam wamepoteza dira na matumaini ya kufanikiwa katika maisha. Wengine ni wahitimu wa vyuo vikuu, shule za sekondari na zaidi ni kwamba wana vipaji tofauti ambavyo kwa namna moja ua nyingine vipaji vyao vingetumika vema basi taifa lingepiga hatua kiuchumi, kisiasa na kijamii. Badala yake vijana hawa wamejiingiza katika urahibu wa madawa ya kulevya na hatimaye 'KUKATA RINGI' na pengine wameambulia kukamatwa na kusweka rupango kila mara hali inajulikana fika kwamba vijana hao hawana uwezo wa kwenda Pakistan, Hong Kong, Trinidad au Malaysia kwenda kufata madawa ya kulevya, je wahusika wakuu wa shughuli hii hawafahamiki daima?

Tuyaache hayo, katika kutembea kwangu nimejionea namna ambavyo mji wa Geita umejaa siasa za maji taka na ukiritimba uliozidi, mpaka leo mji huu hauna maji safi na salama achilia mbali japo kiwanda cha kutengeneza jojo ili vijana wapate ajira baada ya maeneo waliyokuwa wakichimba dhahabu kupewa wawekezaji. Sina lawama sana kwa vijana wengi waliojiingiza katika biashara ya mkaa na kufilisi miti karibia yote katika msitu wa Kukuluma. Potelea mbali mabadiliko ya hali ya hewa maana hakuna namna, ndivyo wasemavyo vijana wengi.


Yote tisa, kumi ni kuhusu jambo moja ambalo limenisumbua kwa miaka karibia 24 na leo nimeamua niliweke bayana. Kuna mtu mmoja huwa ninakutana nae kila pahala ninapotembelea na sielewi kama huwa ananifuatilia kwa siri au basi tu tunakutana kwa bahati mbaya kama vile ambavyo eneo la vwawa lilikutana na kimondo hapa duniani kule wilayani Mbozi.
Awali, nilikutana na jamaa huyu eneo la bonde la Mwakaleli kule mkoani Mbeya. Cha ajabu huyu ni mtu maarufu na karibia koo zote wanamjua huyu jamaa kuanzia kwa Mwasandube, Mwalugaja, Mwambope, Mwangela, Mwandosya, Mwakatuma, Mwakilasa, Mwangosi na hata ukoo wa Mwasanguti wanamjua vema mtu huyu anayependa kunifuatilia. Sijui kama amejiajiri au ameajiriwa kunifuatilia ila niseme ukweli tu kwamba nina mashaka makubwa kuhusu mtu huyu haswa kwa huu mwaka wa uchaguzi.
Image result for pictures of Nape Nnauye
Mhe.Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM

Kwa kule Mwakaleli nakumbuka walikuwa wanamuita "Silule". Hili ni jina la kejeli likimaanisha mtu anayejifanya anajua kila kitu, hashauriki na hata akishauriwa leo basi kesho atarudia makosa yale yale. Pamoja na sifa nyingi anazojipamba nazo Silule, sifa yake kubwa ni kudharau wengine na kupuuza yajayo hivyo ana kasumba ya kuropoka pasipo kupima athari ya maneno yake siku za mbeleni.
Sasa kasheshe ni pale Silule anapokabidhiwa dhamana ya uongozi au cheo, hakika ataapa kutawala milele tena kwa hila zote ili mradi tu anawapa wakubwa zake wanachokipenda pasi na kujali haja ya anaowaongoza au kuwatumikia. Huyo ndiye Silule. Baada ya kuivumilia kwa kipindi kirefu tabia yake, nilifanya maamuzi magumu kuliko yale maamuzi magumu ya fisadi anayejiuzulu bila kushitakiwa. Na laiti kama ningekuwa nazungumza na vijana wenzangu wa pale Isanu, Tunduma basi ningesema..."Nakhatele ni nene sya silule" yaani nilichoka na maudhi ya Silule.

Niliamua kusafiri kwenda mbali kabisa na mkoa wa Mbeya nikiamini kwamba kamwe Silule hatanifuata huko lakini kumbe nilikuwa naota ndoto za Alinacha. Siku moja nikiwa uhamishoni huko Bukoba mjini, gafla nikamwona Silule ambaye kama si yule niliyemwacha Mbeya miaka kadhaa iliyopita basi wanafanana mwili, sauti, nguo na hata akili tena kwa asilimia mia moja. Ilikuwa mwezi uliopita, Silule alivalia shati kama kombati hivi lenye rangi ya kijani. Nilimuuliza Mzee Byera kuhusu vazi lile, alinijibu kwamba huenda mhusika ameamua kuvaa vile ili aendane na rangi ya migomba yaani ule ukijani. Wala sikumwambia kama ninamfahamu mtu yule.

Kivumbi kilikuwa siku ya kesho yake ambapo Silule alikuwa mmoja kati ya wazungumzaji katika mkutano wa hadhara, unaweza ukatabiri alisema nini?
Hapana, najua wewe si mtabiri wa hali ya hewa ila Silule alisema eti waliotuhumiwa kujiandikisha mara mbili katika daftari la kudumu la wapiga kura huko Njombe na maeneo mengine ya nchi ni wale wanachama wa vyama vya upinzani sana sana wana-UKAWA. Usiniulize kama alijuaje maana jibu sina maana hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuthibitisha shutuma hizo, kibaya zaidi ni pale ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Damian Lubuva alipokataa kuwa taarifa hizo ni za kweli na zimetolewa na ofisi yake. Jaji Lubuva alisema ni kweli kuna watu wamekamatwa kwa kosa hilo lakini haijulikani ni wa chama gani.

Tuliporudi nyumbani Mzee Byera alikuwa amenuna mno, nikamhoja kulikoni? Alinijibu, "Yule Kangambeyo nilidhani ataongea mambo ya maana kumbe shutuma za kitoto na propaganda za kizamani loh". Hapo sikuuliza swali lingine maana niling'amua kiutu uzima kwamba kumbe yule Silule wa Unyakyusani akiwa huku Uhayani anaitwa Kangambeyo. Binafsi nilikereka sana na siku hiyo hiyo nikafungasha virago kwenda Mwanza ili nisije kumwona tena wala kusikia tena maneno ya Kangambeyo. 
Na ili azma yangu itimie sikutaka kukaa katikati ya jiji la Mwanza, nikaenda mpaka kijiji cha Igombe kilichopakana na kambi ya jeshi ya Igombe kama kilomita mbili kutoka airport. Cha ajabu nilipofika tu Igombe ilikuwa siku ya jumatano kulikuwa na gulio, nikakutana tena na huyu jamaa. Nahisi alikuwa ananifuatilia, stori za kila kijiwe zilimhusu huyu Silule au Kangambeyo ila niligundua kwamba kumbe alipokuwa huko Usukumani anaitwa Mushilimu ila ni mtu yule yule mmoja. 

Kimsingi nina maelezo ya kujaza kurasa nyingi za kitabu kumhusu Silule au Kangambeyo au Mushilimu ila sasa naomba maelezo yake yaishie hapo ili niende kwenye kiini cha makala hii.
Wiki kadhaa zilizopita, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Moses Nnauye alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema kwamba, "CCM kitashinda katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais utakaofanyika mnamo oktoba 25, 2015 hata kwa goli la mkono". Kimsingi kauli hii imewakera wananchi wengi wanaopenda demokrasia ya kweli na uchaguzi uliohuru na haki. Na ninaamini nikimpigia simu Mzee Mwatogile kule Unyakyusani atasema kauli hiyo imetolewa na Silule, nikimpigia simu Mzee Rutashobya kule Uhayani atasema mtoa kauli hiyo ni Kangambeyo na bila shaka Mzee Masanja wa Usukumani atasema mtoa kauli hiyo ni Mushilimu.

Wakati asasi za kiraia, taasisi za dini na wanaharakati wakihamasisha watu wajiandikishe ili wapate viongozi bora, makini na wasiokumbatia ufisadi, Nape Nnauye anasema kazi hiyo ni bure maana CCM watashinda kwa namna yoyote ile. Na ni kweli, nimepata kushuhudia maeneo kadhaa mabalozi wa CCM wanaenda na madaftari yenye majina ya watu katika vituo vya kujiandikisha wapiga kura. Si tu kwamba mabalozi wa CCM siyo watendaji wa tume ya taifa ya uchaguzi bali pia kuna utata kuhusu majina wanakoyatoa tena siku ya kwanza ya kujiandikisha. Binafsi niliwaona mabalozi wawili Mzee Rusheke katika kituo cha shule ya msingi Mkoani na Mzee Duwa katika kituo cha shule ya msingi Nyanza. 
Unashangaa, sisemi hilo ndilo goli la mkono la Mhe. Nape ila inaweza kuwa sehemu ya kile ambacho kwenye mpira kinaitwa 'counter attack' kuelekea goli la mkono.
Vijana wa Red Brigade wa CHADEMA wakionesha heshima zao kwa Mwenyekiti wa chama Mhe.Freeman Mbowe

Kinachonitia hofu zaidi ni mantiki ya goli la mkono, mfano wanachama wawili wa CUF wamepigwa risasi katika eneo la kujiandikisha katika eneo la Makunduchi huko Zanzibar. Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Arahma, ni kweli wahusika hawajulikani lakini itakuwaje watu wakihusianisha tukio hilo na harakati za goli la mkono?
Kwa kuwa Mwenyekiti wa CCM pia ndiye Amiri Jeshi Mkuu na mara kadhaa tumeshuhudia wakuu wa mikoa na wilaya wakitoa amri kwa wanausalama haswa jeshi la polisi, je kwanini tusiwe na hofu kwamba yeyote atakayelipinga goli la mkono atapigwa au kubambikiziwa kesi? Pia, tunahoji kama wapinzani wapo tayari kufungwa goli la mkono?
Kwa nini nisiwe na hofu wakati najua kwamba maadui wa ndani na nje wanaweza kutumia njia ile ile ya goli la mkono kujipenyeza katika uwanja wa kuzua fujo, uhasama na mauaji katika taifa? Pengine, jambo linalotia simanzi ni ukimya wa Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais aliyeapa kuitumikia na kuilinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tuamini kwamba haoni hatari katika kauli iliyotolewa na katibu mwenezi wa chama chake?
Kama ndivyo basi mimi sitaki bughudha, wiki ijayo naanza safari ya kwenda mafichoni huko Garissa, Kenya kwa Mhe.Uhuru Kenyatta potelea mbali Alshaabab maana afadhali adui anayejulikana kuliko kusubiri tukio la goli la mkono litakalofungwa na Silule, Kangambeyo au Mushilimu. Refa kateuliwa na bosi wa Mushilimu hivyo haki haitakuwepo na bila haki amani haidumu.
Kwaheri ya kuonana!

MAJINA YA WALIOFICHA FEDHA USWISI NI UTATA MTUPU, ZITTO ADAIWA KUONGOPA

 
 
Pamoja na mambo mengine yaliyozungumzwa na Mhe.Zitto Ayatollah Kabwe katika hotuba yake katika viwanja vya Mwembeyanga hapo jana ni kuhusu Watanzania walioficha fedha nchini Uswisi. Kutoka mwaka 2012 ilipotoka ripoti ya bunge ya kuitaka serikali kuchunguza majina ya Watanzania walioficha fedha nje ya nchi, kulikuwa na hoja kubwa mbili ambazo hazijathibitishwa kwa namna yoyote ile na kile kinachoitwa Zitto kuwataja majina Watanzania walioficha hela nje ya nchi.
Awali ya yote ieleweke wazi kuwa si dhambi kwa Mtanzania kuwekeza au kuhifadhi fedha nje ya nchi hivyo hoja ni sifa na uhalali wa fedha hizo. Kwa muktadha huo kile kichokuwa kinatizamwa kwa kipindi kirefu ni aidha fedha hizo ni umma na zimefanyiwa mchezo wa kifisadi na baadhi ya watendaji waandamizi wa serikali walioamua kwenda kuficha fedha hizo nje ya nchi ili kijinasua na uchunguzi wa tume ya maadili ya viongozi wa umma au usalama wa taifa (TISS). Pili, hoja kubwa ilikuwa kwamba fedha hizo ni faida ya uhujumu uchumi miongoni mwa Watanzania jambo ambalo Mhe.Zitto Kabwe ameshindwa kutueleza. Rejea aya hii iliyopo katika hotuba yake:
 


"Fedha hizi zaweza kuwa halali ama haramu. Kuna watu ama ni Watanzania wanaishi ughaibuni na kufanya kazi huko ni lazima wawe na akaunti za benki. Pia kuna Watanzania ambao ni wafanyabiashara na masharti ya biashara zao ni lazima wawe na akaunti katika mabenki ya nje. Hata hivyo mfumo mzima wa ufunguaji na ufungaji wa akaunti katika mabenki ya nje umewekewa masharti ya kisheria na kibali cha Benki Kuu kinahitajika. Kuna Watanzania wenye kuficha fedha ambazo zimepatikana kwa rushwa na biashara haramu mbalimbali kama vile madawa ya kulevya na biashara ya nje ambayo haingii kwenye rekodi za Benki Kuu. Iwapo Serikali ingefanya uchunguzi na kuukamilisha tungeweza kujua kwa hakika katika orodha ya watu wenye akaunti nje ni wepi wana fedha zao halali na wepi wana fedha haramu. Serikali imetunyima haki hiyo kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa. Bunge la Kumi linavunjwa mnamo tarehe 9 Julai mwaka huu na hakuna dalili yeyote ya Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi ndani ya bunge kama ilivyoagizwa na Bunge."

Kumbe alichokifanya Mhe.Zitto ni kuendeleza maisha ya tetesi badala ya kuutafuta ukweli. Toka mwaka 2012 alitakiwa kuwataja wahusika lakini akafyata mkia, je alisubiri zibaki siku 5 za kulivunja bunge ndipo awataje wahusika?
 


Pia jambo linalotia wasiwasi ni majina ya watajwa, je hakuna Watanzania wengine nje ya wenye majina ya kiarabu na kihindi?
Tatu, uhalali wa majina hayo ni upi maana hayaeleweki yametoka taasisi gani ya kiuchunguzi ama benki husika ili tuamini kuwa ni ya kweli, vile vile TAKUKURU na TISS wapate msaada wa kuutafuta ukweli?
 

 
Nne, kwanini Mhe.Zitto Ayatollah asisome mwenyewe majina hayo ili awe sehemu ya ushahidi kama alivyowataja Dr.Willbrod Slaa katika List Of Shame, badala yake Zitto akawapa waandishi majina ambayo si tu kwamba yanamuweka mbali na ushahidi bali pia hayana sahihi yake. Kwa ujumla majina yaliyotajwa na Mhe.Ayatollah kama ambavyo wachambuzi wengi wamechambua, hayajatibu kiu ya watanzania waliotaka kufahamu ukweli wa jambo hili. Zitto anatakiwa kujipanga upya vinginevyo umma utazidi kupoteza imani kwa mwenendo wa siasa za aina hii.