MHE.JAMES MBATIA |
HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA
FEDHA MHESHIMIWA JAMES FRANCIS MBATIA (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO
NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
(Inatolewa Chini ya Kanuni ya 105(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Mwaka 2013)
(Inatolewa Chini ya Kanuni ya 105(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Mwaka 2013)
I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa siha njema ya kuweza kusimama mbele ya Bunge hili ili niweze kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KRUB), kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2015/2016 chini ya Kanuni ya 105 (8) ya Kanuni za kudumu za Bunge , toleo la Mwaka 2013.
2. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, napenda kutoa shukrani za dhati kwa kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni; Naibu Waziri Kivuli wa Fedha, Mhe. Christina Lissu Mughwai (Mb); Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri vivuli kutoka katika KRUB na kwa viongozi wengine wote wa vyama vya siasa vilivyoasisi Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakiongozwa na Wenyenyeviti wenza Ndugu Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) - CHADEMA, Ndugu Prof. Ibrahim Haruna Lipumba-CUF na Ndugu Dkt. Emmanuel Makaidi-NLD kwa ushauri na maoni yao yaliyofanikisha kuandaa hotuba hii.
3. Mheshimiwa Spika, Katika nchi yenye mfumo wa Demokrasia na Utawala bora, ambapo viongozi wa Serikali wanachaguliwa katika chaguzi zilizo huru na za haki, Sera ya Maendeleo ya Taifa ni mkataba kati ya Serikali na wananchi; mkataba unaosimamiwa na nguvu ya wananchi waliowachagua na wasiowachagua. Serikali ikishindwa kutimiza mkataba huo, wananchi hutumia nguvu ya uchaguzi kuiondoa madarakani.
4. Mheshimiwa Spika, Bajeti ni nyenzo muhimu ya sera ya maendeleo ya Serikali yoyote. Bajeti ni kielelezo cha maeneo ambayo Serikali inayapa kipaumbele katika ustawi wa maisha ya wananchi wake, kwa ujumla. Serikali hukusanya mapato toka kwa walipa kodi, kwa uadilifu; na kupanga kutumia mapato hayo, kwa uangalifu; katika maeneo yatakayostawisha jamii nzima. Kinyume na matarajio ya wengi, Serikali hii imeshindwa kutimiza malengo yake, ikiwemo kukusanya kodi bila uadilifu na hivyo kuchochea vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu. Haya ni matokeo ya kushindwa kwa sera, ilani, mikakati, utendaji na uendeshaji wa Serikali inayondoka madarakani.
5. Mheshimiwa Spika, Ustawi wa jamii ni tunda la Uchumi stahimilivu; ni bahati mbaya kuwa Serikali hii imeshindwa kutimiza ahadi yake ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake jamii ya Kitanzania sasa inashuhudia kwa kasi, ongezeko la mfumuko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni na kuporomoka kwa thamani ya sarafu yake. Kuyumba huku kwa uchumi, kumewaumiza watanzania wa makundi yote.
6. Mheshimiwa Spika, kupanga ni kuchagua. Kupanga vizuri ni kuchagua vizuri. Hali kadhalika, kuchagua vibaya ni kupanga vibaya. Bajeti nayo ni mpango mpana wa mapato na matumizi ya kuendeshea jamii yoyote, iwe ni jamii ndogo au kubwa. Bajeti, kwa namna nyingine, ni nyenzo mojawapo kuu ya uchumi stahimilivu na ustawi wa jamii.
7. Mheshimiwa Spika, kutokana na takwimu za Benki Kuu za Juni 2014 na Juni 2015, thamani ya shilingi moja ya Juni mwaka jana inazidi shilingi 1.2 ya leo. Kwa hiyo shilingi trilioni 19.8533 za Juni 2014 thamani yake kwa sasa ni zaidi ya shilingi trilioni 24 za leo.
Jedwali I
Mwaka Thamani ya USD Bajeti (Milioni)
dhidi ya Shilingi Shilingi USD
2014/2015 1,650.00 19,853,331.00 12,032.32
2015/2016 2,066.00 22,495,493.00 10,888.43
Chanzo: Benki Kuu ya Tanzania (Thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani)
8. Mheshimiwa Spika, tofauti kati ya mwaka 2014/2015 na 2015/2016 ni Dola milioni 1,143.89. Sawa na Shilingi trilioni 2,363,283,876,000.00. Punguzo hili ni sawa na asilimia 9.5 Hivyo, leo Serikali inapojingamba kuwa bajeti imeongezeka kutoka shilingi trilioni 19.8533 kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 kufikia shilingi trilioni 22.495 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 siyo sahihi. Kwani inasahau kuwa, thamani ya shilingi ya leo ni pungufu ya thamani ya shilingi ya mwaka jana. Hii ina maana kuwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2015/2016 ni ndogo kuliko bajeti ya mwaka 2014/2015. KRUB, inasikitishwa na kitendo cha Serikali kushindwa kuwaeleza watanzania ukweli wa ongezeko hasi la bajeti ambalo haliendani na thamani ya Shilingi kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016. Kitendo cha Serikali hii kuwadanganya watanzania kwa kuwapa tumaini hewa la ongezeko la bajeti ni cha kupingwa kwa nguvu zote na watu wote kwa manufaa ya Mama Tanzania.
9. Mheshimiwa Spika, inafahamika kwamba sababu mojawapo ya kuporomoka kwa thamani ya shilingi ni tabia ya kifedha iitwayo “dollarization”, inasikitisha kuona kwamba Serikali nayo inakubaliana na hali hiyo ambayo ina madhara na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa letu masikini. Rejea aya ya 12, uk. 11; aya ya 80, uk. 64; aya ya 82, uk.67; aya ya 84, uk. 73; na aya ya 88, uk.78. Hotuba ya Bajeti ya waziri wa fedha ya mwaka 2015/2016.
Matatizo na changamoto za mfumo wa bajeti uliopo
10. Mheshimiwa Spika, Matatizo yaliyopo ni ukosefu wa nidhamu na uwazi katika masuala ya bajeti. Kipindi hiki Taifa linashuhudia uwepo wa ongezeko la malimbikizo ya malipo; bajeti inayopitishwa na Bunge haifanani na bajeti inayotekelezwa na Serikali ; Makadirio ya mapato ni makubwa kuliko ukusanyaji wa mapato halisi; ongezeko holela la misamaha ya kodi; bajeti tegemezi; Matumizi ya kawaida ni makubwa kuliko mapato ya serikali; matumizi ya kawaida ni zaidi ya fedha za miradi ya maendeleo; Kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa deni la taifa; ongezeko la vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yanaainishwa na CAG lakini hakuna hatua za kisheria na za kinidhamu stahiki zinazochukuliwa. Kipindi hiki tunashuhudia wagombea zaidi ya 30 wanaotaka Urais kwa ticketi ya CCM wakishindana kukosoa chama chao wakijinasibu watafufua uchumi, wakati wao ni sehemu ya mfumo huo huo uliodumaza uchumi wetu. KRUB, inawatahadharisha Watanzania kutokukubali kudanganywa tena.
11. Mheshimiwa Spika, ni muhimu kutambua kuwa sera na sheria peke yake haziwezi kuleta mabadiliko ya msingi. Serikali hii imekuwa na utamaduni wa kutoheshimu na kutekeleza sera na sheria zilizopo. Na ndio maana badala ya kutekeleza sera na sheria za nchi serikali imekua ikibadilisha kauli mbiu zake huku tukishuhudia pengo kati ya walionacho na wasiokuwanacho likizidi kuongezeka.
Misingi ya Bajeti
12. Mheshimiwa Spika, katika kurudisha misingi bora ya bajeti ya Serikali, tunaamini kuwa Serikali ijayo chini ya UKAWA itarudishsa nidhamu ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato na kuhakikisha yafuatayo yanatekelezwa;
(i) Kwa ujumla mapato yote yakusanywe na matumizi kupangwa bila kujali chanzo cha mapato, ikiwa kuna mahusiano ya karibu kati ya mapato na wanaonufaika na matumizi ya mapato hayo, hoja ya mapato husika kulipia matumizi ya huduma inakubalika.
(ii) Maamuzi ya Serikali na viongozi ambayo yanahitaji matumizi ya fedha za Serikali katika mwaka wa bajeti au miaka ijayo yanawekwa wazi na kuchambuliwa.
(iii) Utayarishaji wa bajeti utakaozingatia :-
a) Kufikia malengo ya uchumi mpana kwa kusimamia ukuaji wa pato la taifa, udhibiti wa mfumuko wa bei, akiba ya fedha za kigeni, thamani ya sarafu.
b) Matumizi yagawiwe kulingana na malengo ya sera ya taifa.
c) Kujenga mazingira ya utekelezaji mzuri wa bajeti.
13. Mheshimiwa Spika, Jambo kubwa ambalo limekuwa likiathiri sera, utayarishaji na utekelezaji wa bajeti bora ni uanzishaji wa sera na ahadi kwenye majukwaa ya siasa ambayo hayaendani na vipaumbele vilivyotumiwa kuandaa bajeti. Yafuatayo yatatekwelezwa na Serikali makini ya UKAWA:
i. Kuratibu vizuri uanzishaji wa sera
ii. Kushirikisha umma katika kuanzisha sera
iii. Kuwa na utaratibu mzuri wa kupitia na kutathmini sera na bajeti za Serikali katika bunge.
iv. Uchambuzi wa kina wa mahitaji ya fedha na rasilimali nyingine za mapendekezo ya bajeti.
v. Kuhakikisha kuwa bajeti ndiyo inayoshika hatamu katika mapato na matumizi ya Serikali.
vi. Maandalizi ya bajeti yatakayozingatia hali halisi ya uchumi. Ni muhimu kuwa na makadirio sahihi ya mapato na kuyatambua matumizi yote ya lazima.
II. UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA WA 2014/15
14. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri ukweli kuwa, Serikali ya CCM hamjawatendea haki watanzania kwa kuwa wakati Serikali imetegemea kukusanya mapato ya shilingi trilioni 10.3 badala ya 11.3 ya lengo la awali la ukusanyaji wa mapato. Mapato yasiyo ya kodi yatakuwa chini ya malengo kwa shilingi bilioni 223.6 na mapato ya halmashauri yatakuwa chini ya malengo kwa shilingi bilioni 100.9. Ukusanyaji wa mapato ya ndani ikijumlisha mapato ya halmashauri yatakuwa chini ya malengo kwa shilingi trilioni 1.34 sawa na asilimia 11 ya malengo ya bajeti.
15. Mheshimiwa Spika, kutokana na kashfa ya ufisadi wa Tegeta Escrow Account wahisani walisitisha misaada ya bajeti kwa hoja kuwa viongozi wa serikali walipanga na kufanikisha mbinu za kuliibia shirika la umma la TANESCO lenye matatizo makubwa ya kifedha. Walipa kodi wa nchi zao hawatakubali kuendelea kuipa misaada serikali ya namna hiyo. Mpaka kufikia mwezi Aprili 2015, wahisani walikuwa wameipa serikali mikopo na misaada ya kibajeti ya shilingi bilioni 406 ukilinganisha na ahadi ya shilingi bilioni 922 sawa na asilimia 40. Serikali imepokea Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendeleo shilingi trilioni 1.4 ukilinganisha na bajeti ya shilingi trilioni 2.0 sawa na asilimia 70 ya bajeti.
16. Mheshimiwa Spika, mikopo yenye Masharti ya Kibiashara haikupatikana kama serikali ilivyotarajia. Serikali ilitarajia kukopa Dola milioni 800 lakini mpaka Aprili 2015 ilifanikiwa kukopa Dola milioni 300 tu sawa na asilimia 39 ya kiwango kilichowekwa kwa mwaka mzima. Lakini swali la kujiuliza, kwenye nchi yenye rasilimali za kutosha inawezaje kuweka mikopo kama mojawapo ya kipaumbele cha vyanzo vya uendeshaji wa Bajeti yake? Hili ni jambo la aibu kubwa, kuona kuwa Serikali inashindwa kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa kuwa walipoomba kukopa, mikopo hiyo haikutolewa. Athari za mikopo holela ya Serikali huishia kuwa mizigo kwa wananchi wote.
17. Mheshimiwa Spika, bajeti ya maendeleo ndiyo imeathirika sana. Mpaka kufikia Aprili 2015 matumizi katika bajeti ya maendeleo yalikuwa asilimi 40 tu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Katika kipindi hicho matumizi ya kawaida yalikuwa asilimia 86 ya bajeti ya mwaka mzima. Swali la kujiuliza, unaendeshaje uchumi ambao hauna fedha za miradi ya maendeleo lakini fedha za mishahara na posho zinaendelea kulipwa? Hii inamaanisha kuwa pia kiwango cha uzalishaji wa huduma nchini kinapungua. Inasikitisha kuona kuwa Serikali inaendesha nchi bila tija na manufaa kwa watu wake wenyewe.
18. Mheshimiwa Spika, miradi ambayo imewekwa chini ya BRN – Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ambayo serikali inasema inaipa kipaumbele imeathirika kwa kiwango kikubwa. Hadi kufikia Aprili, 2015 “shilingi bilioni 649.5 zimeelekezwa kwenye mafungu yanayotekeleza miradi ya Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” lakini katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha wa 2013/14 Waziri alieleza “hadi kufikia Aprili, 2014, mafungu yanayotekeleza miradi ya BRN yamepatiwa jumla ya shilingi bilioni 1,566.7 sawa na asilimia 92 ya bajeti ya miradi ya BRN kwa mwaka 2013/14”. Fedha zilizotumiwa kwenye miradi ya BRN mwaka 2014/15 ni asilimia 41 ya fedha zilizotumiwa mwaka 2013/14. Leo mnaposema mmefanikiwa kwa kupitia BRN, ni vigezo vipi ambavyo mnatumia kujipima navyo?
19. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa pamoja na Serikali kuendelea kubadilisha kauli mbiu na mipango ya kuendesha miradi ya maendeleo, miradi hii haiwezi kufanikiwa chini ya Serikali ya CCM kwa kuwa wamekua na mipango mingi. Tatizo lingine lipo kwenye usimamizi na kukosekana kwa wengi wenye moyo wa dhati, utashi, maadili na hata uthubutu wa uwajibikaji katika kusimamia mipango yenye manufaa kwa umma.
20. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya bajeti (HB) ya mwaka 2014/15, KRUB, ilitoa mapendekezo ya kuboresha ufanisi wa bajeti hiyo. Baadhi ya mambo hayo ambayo tuliyapendekeza ni pamoja na ;
(i) Kutoa unafuu wa kodi kwa viwanda vya nguo na ngozi, ili kuvifufua, rejea aya ya 63 – 65, uk. 27 wa HB 2014/15 ;
(ii) Kuzingatia kiwango cha chini cha fedha za bajeti katika miradi ya maendeleo, asilimia 35, kama ilivyo kwenye mpango wa kwanza wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano;
(iii) Kutekeleza na kuweka wazi hatua zinazopangwa katika kukabiliana na mtu yeyote anayebainika kufanya ubadhirifu au kujihusisha na rushwa katika kufanya manunuzi ya umma;
(iv) Kushirikiana na sekta binafsi ili kuweka mikakati ya kuwa na bajeti itakayopanua sekta hiyo; kwa ajili ya kuongeza ajira;
(v) Kuongeza vyanzo vya mapato; kwa kuboresha ukusanyaji wa kodi, rejea aya ya 66 – 67, uk, 28, HB 2014/15;
(vi) Kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa kupitia : (a)uwekezaji wa Kodi, (b) vivutio vya kodi katika sekta ya madini, (c)kupunguza misamaha ya kodi kwa kutoa misamaha hiyo kwa wawekezaji wa kimkakati, na (d) kudhibiti na kuzuia upotevu wa mapato katika sekta ya madini; rejea aya ya 69 – 77, uk. 30-34, HB 2014/15; na
(vii) Kuweka maanani, kwa vitendo, thamani ya muda wa wananchi katika kutumia miundombinu ya kupata huduma za kijamii kama vile afya, maji, elimu, na usafiri.
21. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/15, KRUB ilikumbushia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa kwa Serikali katika mwaka 2013/14.
(i) Kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi kwa kuunda mfumo wa kuoainisha, kwa kila mwananchi, kitambulisho chake cha Taifa na namba yake ya kulipa kodi (TIN Number). Mfumo huu, utamsaidia kila mwananchi kuwajibika kujaza fomu za taarifa za kodi (tax return) bila kujali kipato chake na hivyo kupunguza mianya ya ukwepaji kodi;
(ii) Kuweka wazi misamaha yote ya kodi ili kupunguza ukwepaji wa kulipa kodi;
(iii) Kuanzisha Chuo Kikuu Mtwara, cha kutayarisha wataalam stahiki katika sekta ya Mafuta na Gesi; ili kuweza kutumia utajiri wa rasilmali husika uliopo nchini; na
(iv) Kurekebisha Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004; kwa kufuta sehemu ya Kodi ya Mapato inayotoa fursa kwa kampuni za madini kutumia sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973, iliyofutwa (grandfathering). Pendekezo hili bado halijatekelezwa kwa Kampuni za madini zenye mikataba.
22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15, KRUB ilitoa mapendekezo yafuatayo kwa Serikali;
(i) Kupunguza matumizi ya kawaida kama ilivyoelezwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano, ibara ya 4.5.1;
(ii) Kuweka wazi madeni ya kila sekta ili kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima; na
(iii) Kutekeleza na kuweka wazi hatua zinazopangwa katika kukabiliana na mtu yeyote anayebainika kufanya ubadhirifu au kujihusisha na rushwa katika matumizi ya umma, rejea aya ya 44 na 47, uk. 21 -22, HB 2014/15
23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15, KRUB ilikumbushia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa kwa Serikali katika mwaka 2013/14 ikiwemo;
(i) Kuacha kuchukua mikopo yenye masharti ya kibiashara;na
(ii) Kupiga mnada baadhi ya magari ya Serikali, ili matumizi ya serikali yaendane na pato la taifa.
24. Mheshimiwa Spika , katika mwaka wa fedha 2013/14, KRUB, ilipendekeza yafuatayo kwa Serikali;
(i) Kuweka maanani, kwa vitendo, thamani ya muda wa wananchi katika kutumia miundombinu za kupata huduma za kijamii kama- matibabu, maji, elimu, na usafiri.
(ii) Kuweka kipaumbele kwenye hospitali za Serikali na kuhakikisha zinatoa huduma stahiki kwa ujumuisho; na
(iii) Kuweka kipaumbele kwenye mpango wa Kilimo kwanza, ili kupata hifadhi ya kutosha ya chakula kwa jamii nzima.
25. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2014/15, KRUB, ilikumbushia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa kwa Serikali katika mwaka 2013/14 ikiwa ni pamoja na;
(i) Kushusha kiwango cha kodi ya mapato kwa wafanyakazi kutoka asilimia 14 hadi asilimia 9; rejea aya ya 6(e), uk. 4, HB 2014/15; Lakini Serikali imeshusha kiwango hicho kuwa asilimia 11. Swali la kujiuliza, je punguzo hilo la PAYE linampa unafuu mfanyakazi katika muda ambao gharama za maisha zimepanda na mishahara yao imeendelea kuwa duni? Rai yangu kwa wafanyakazi wote nchini, kuhakikisha kuwa wanafanya maamuzi sahihi kwa kuwachagua viongozi watakaoweza kutetea maslahi yao na si kuwachagua viongozi ambao wanatumia shida zao ujipatia uhalali wa kubaki madarakani.
(ii) Kuanzisha pensheni ya Uzeeni, kwa wazee wote nchini; labda kwa masikitio makubwa tuungane na wazee wote nchini ambao ni hazina ya taifa, kupinga hadaa na laghai ya kisiasa inayofanywa na Serikali hii. Ikumbukwe kuwa pamoja na kupitishwa kwa Sera ya Wazee, kauli mbalimbali zimetolewa kuwa pensheni kwa wazee haiwezekani. Kauli ya waziri wa fedha kuwa ipo kwenye mchakato wa upembuzi wa idadi ya wazee tena kwa mwaa 2015/2016, ni muendelezo wa kuwajengea wazee hawa matumaini kuwa watapewa mafao huku Serikali ikijua haiwezi kutekeleza ahadi hiyo iliyotolewa kisiasa.
(iii) Kushusha tozo la kuendeleza stadi kutoka asilimia 6 hadi asilimia 4; rejea aya 6(n), uk. 7, HB 2014/15
26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15, KRUB, ilipendekeza yafuatayo kwa Serikali:
(i) Kuacha kutumia mikopo ya kibiashara kulipa deni la taifa;
(ii) Kuboresha uwiano kati ya fedha zinazotumika kulipa madeni ya hati fungani na fedha zinazotumika ajili ya miradi ya maendeleo;
(iii) Kudhibiti kiwango cha ukuaji wa deni hilo; kutokuzidi kiwango cha ukuaji wa uchumi; na
(iv) Kutoa taarifa za maendeleo yanayotokana na mikopo hiyo inayokinzana na kanuni anuai za kiuchumi, ili kukabili deni hilo.
27. Mheshimiwa Spika, KRUB ilitarajia kuona bajeti yenye uhalisia wa kujali utu wa kila mtu nchini; rejea aya ya 19, uk. 11. Bajeti ya aina hiyo hulenga:
(i) Kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi;
(ii) Kutengeneza ajira stahiki kwa wananchi;
(iii) Kukuza uwekezaji hasa wa ndani;
(iv) Kumwezesha mwananchi kuweka akiba;
(v) Kuinua maisha ya waishio vijijini, kwani ndio walio wengi;
(vi) Uchumi wa nchi kumilikiwa, kwa asilimia kubwa, na wananchi;
(vii) Kukuza ujasiriamali; na
(viii) Kukuza ulaji na uzalishaji endelevu (Promote sustainable consumption and production).
28. Mheshimiwa Spika, kuhusu Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa miaka 5, KRUB ilitoa maoni kwamba mpango huu haukufanikiwa ipasavyo kwa kukosekana kwa sera ya utekelezaji wake; rejea aya ya 26 -36, uk. 16 – 19, HB 2014/15.
29. Mheshimiwa Spika, kuhusu Sekta Binafsi na Ajira kwa Vijana, KRUB ilitoa maoni kwamba manufaa ya Sekta Binafsi na ajira kwa vijana, ni zaidi ya mapato kwa jamii na kwa mtu binafsi. Manufaa yake ni pamoja na kukuza utambuzi wa Utu wa mwanadamu na kukuza amani duniani; rejea aya ya 37 – 41, uk. 19 -20, HB 2014/15. Leo hii sekta binafsi inaendelea kukuza uchumi wa Taifa lakini Serikali inashindwa kuoanisha mipango yake kuhakikisha kuwa wazawa wanapewa kipaumbele katika kuingia ubia na Serikali kupitia PPP na hivyo kuimarisha ustawi wa jamii yake hasa katika utoaji wa huduma muhimu ikiwemo afya, elimu, nishati, maji na kadhalika. Aidha, ongezeko la ukosefu wa ajira nchini hauendani na maelezo ya waziri kuwa Serikali imeongeza ajira nchini kutokana na ukuaji wa uchumi huku takribani watanzania milioni 20 wakihesabiwa kuwa nguvukazi ya Taifa. Asilimia kubwa ya nguvu kazi inajihusisha na kilimo na pia kwenye sekta isiyo rasmi, je ni kwa kiwango gani Serikali imeinua kilimo na kuiwezesha sekta isiyo rasmi kuinua uchumi?
30. Mheshimiwa Spika, kuhusu Vipaumbele vya Taifa, KRUB ilitoa rai kwa Serikali ya kuwa na vipaumbele vinavyoendana na malengo ya mipango ya maendeleo ya jumuia, mashirika na taasisi za kimataifa na kitaifa, kama EAC, SADC, AU, UN, IMF na WTO; yanayozingatia maendeleo endelevu ya dunia. Mipango kama MDGs, SDGs, Dira ya Maendeleo ya 2025, Dira ya Maendeleo ya 2063, MKURABITA, MKUKUTA, na Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya miaka mitano; rejea aya ya 42 – 65, uk. 21 – 28, HB 2014/15. Mapendekezo yote kwa miaka minne ya nyuma yanapatikana katika jedwali lililoambatanishwa katika taarifa hii.
31. Mheshimiwa Spika, pamoja na vipaumbele vya taifa kuendelea kubadilishwa kila mara na pia vipaumbele hivyo kutotekelezwa, mipango lukuki ya Serikali inayoingiliana Kisera imeendelea kuongeza gharama za uendeshaji badala ya kutatua changamoto za kiuchumi za watanzania. Hii ina maana kuwa, utitiri wa mipango ya Serikali haujaweza kupunguza makali na maumivu ya kupanda kwa gharama za maisha nchini hali inayosababisha ukosefu wa huduma mbalimbali za kijamii.
III. MAPITIO YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA WA 2015/2016
32. Mheshimiwa Spika, imani ya binadamu ina nguvu ya ajabu. Nitatoa mfano, Mama mwenye upendo wa dhati kwa watoto wake, anaweza kushindwa kuwalisha watoto wake, lakini watoto hawatapoteza imani yao kwake.Watoto wanaweza kuamini mama anachemsha nyama kwenye chungu, kumbe anachemsha jiwe kwa madhumuni ya kuwapa watoto matumaini hadi kuishia usingizini. Watakapoamka itakuwa ni siku mpya na mama atakuwa na uwezo wa kwenda kutafuta chakula.
33. Mheshimiwa Spika, hotuba tunayoijadili ya Serikali ya CCM, imeendeleza dhambi ile ile ya kutumikia mfumo. Tarehe 11 Juni 2015 wakati waziri anasoma hotuba ndani ya Bunge hili, nakala za hotuba hiyo zilicheleweshwa kusambazwa kwa zaidi ya dakika 40, si kwa makosa ya kiuetendaji bali kwa kuwa hotuba ya waziri wa fedha ilijaa mambo yasiyokubalika na Serikali yake wala Chama chake. Pamoja na kuiweka hotuba hiyo viraka vya karatasi na gundi ili visionekane, lakini kwa uwezo wa Mungu tumevisoma na mojawapo wa aibu ya hotuba hiyo ya waziri ni pamoja kwa kielelezo; kusoma maneno yaliyofutwa katika:
➢ Aya ya 12 ukurasa wa 7’ Hata hivyo, uamuzi wa kumuidhinisha kukidhi sifa hizo utafanywa na Bunge. Taarifa za utekelezaji wa uwekezaji huu utapaswa kuwasilishwa Bungeni kila mwaka na waziri mwenye dhamana ya uwekezaji kwa muda wote vivutio mahsusi vitakapokuwa vinatolewa ili kama mwekezaji hatekelezi yale aliyoahidi aondolewe vivutio hivyo.’
➢ Ukurasa wa 44, (e) ili mwekezaji atambuliwe kuwa mwekezaji mahususi waziri mwenye dhamana ya uwekezaji atawasilisha mapendekezo bungeni ili Bunge litambbue hadhi hiyo kupitia azimio;
➢ Ukurasa wa 45, (f) Baada ya mwekezaji kuidhinishwa kuwa mwekezaji mahususi Waziri wa Fedha atawasilisha bungeni mapendekezo ya vivutio mahususi vya kodi; na
➢ (g) Vivutio vitakapotolewa, waziri mwenye dhamana ya uwekezaji atakuwa akiwasilisha bungeni taarifa ya utekelezaji ya uwekezaji huo kila mwaka ili Bunge liweze kuamua endapo vivutio hivyo viendelee au visiendelee.
34. Mheshimiwa Spika, kufutwa kwenye hotuba ya waziri taarifa hii muhimu kwa masilahi ya Mama Tanzania ni wazi Serikali hii ya CCM, hawana uadilifu wa kuwatumikia wananchi kwa uzalendo, umoja, uwazi na uwajibikaji.
35. Mheshimiwa Spika, takwimu zilizomo ni za kutikisa imani ya mwananchi yeyote mwenye kutaka kusoma bajeti na kuielewa. Kuna takwimu za kubabaisha, zinazokinzana, zenye kuonesha maajabu na zenye hadithi za abunuasi. KRUB ina tabia ya kujenga hoja kwa vielelezo. Utafiti umefanyika, takwimu tunazo na ndio vielelezo vyetu, kama ifuatavyo:
a) . Mabadiliko ya Ajabu:
36. Mheshimiwa Spika, Chini ya kipengele cha mwenendo wa matumizi katika mwaka 2014/15, imeripotiwa kwamba hadi Machi 2015, matumizi mengineyo katika matumizi ya kawaida kwenye utekelezaji wa bajeti ni shilingi bilioni 6,811.4 lakini hadi Aprili ni shilingi bilioni 2,726.3; rejea maelezo ya Waziri wa Fedha tarehe 29 Aprili 2015 na aya ya HB ya mwaka 2015/16. Tofauti ya shilingi bilioni 4,085.1 au trilioni 4.0851.Matumizi yaliyotumika hayawezi kuyeyuka.
b) Takwimu Mbili Tofauti:
37. Mheshimiwa Spika, takwimu tofauti:
(i) Kwa kipindi kuanzia Julai 2014 hadi April 2015, mapato ya Serikali za mitaa ni aidha shilingi bilioni 284, au ni shilingi bilioni 296.7; rejea aya ya 28 na 31 ya HB mwaka 2015/16.
(ii) Makadirio ya mikopo na misamaha ya maendeleo kwa mwaka 2014/15 ni aidha shilingi bilioni 2,019.4 au ni shilingi bilioni 1,745.3; rejea HB mwaka 2014/15 na aya ya 33 HB 2014/2016.
c) . Makadirio Yanayokinzana na Takwimu:
38. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa sera ya bajeti ya mwaka 2014/15, Serikali imeripoti kuwa na matarajio kadhaa katika mapato ifikapo tarehe 30 Juni 2015. Matarajio kadhaa hayaeleweki yanatokana na taarifa gani. Kwa mfano;
(i) Wastani wa misamaha ya kodi kwa mwezi hadi Aprili 2015, ilikuwa shilingi bilioni 130.12 lakini Serikali imekadiria wastani wa misamaha hiyo kwa miezi miwili iliyobaki kuwa ni shilingi bilioni 59.15. rejea aya ya 32, uk. 25 HB mwaka 2015/26
(ii) Wastani wa ukusanyaji kodi kwa mwezi hadi hapo Aprili 2015 ilikuwa ni shilingi bilioni 810.65, lakini Serikali ina matarajio ya kukusanya kodi kiasi kinachozidi shilingi bilioni 1,096.5 kwa kila mwezi kwa miezi miwili iliyobaki.
(iii) Serikali ina matarajio ya mapato ya mamlaka ya Serikali za mitaa kuwa ni wastani wa shilingi bilioni 36.185 kwa mwezi wa Mei na Juni, wakati wastani wa mapato hayo hadi Aprili 2015 ilikuwa ni bilioni 28.4 kwa mwezi.
d) . Matumizi ya Kutisha katika Mwezi Aprili 2015:
39. Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili 2015 matumizi yaliyofanywa na Serikali ni makubwa na ya kutisha na ya kutiliwa shaka kwa kuwa;
(i) Wastani wa matumizi ya sekta ya elimu, chini ya mpango wa BRN, kuanzia Julai 2014 hadi Machi 2015 ni shilingi bilioni 2.29; lakini kwa mwezi mmoja tu wa Aprili matumizi yalikuwa shilingi bilioni 106.20.
(ii) Katika mapango huu wa BRN, imeripotiwa:
• Wastani kwa mwezi , sekta ya uchukuzi hadi Machi 2015, ni shilingi bilioni 5.58, lakini kwa mwezi mmoja tu wa Aprili matumizi yalikuwa shilingi bilioni 49.50
• Wastani kwa mwezi, sekta ya kilimo hadi Machi 2015 ni shilingi bilioni 1.2; lakini kwa mwezi mmoja tu wa Aprili matumizi yalikuwa shilingi bilioni 18.0
• Wastani wa matumizi kwa mwezi, kwa mpango huo hadi Machi 2015, ni shilingi bilioni 52.62; lakini kwa mwezi mmoja tu wa Aprili matumizi yalikuwa shilingi bilioni 123.30.
e) . Takwimu Zinazokinzana:
40. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya waziri kuna takwimu zinazokinzana, na hivyo kutilia shaka bajeti hii:
(i) Kwa kipindi kuanzia Julai 2014 hadi Machi 2015, imeripotiwa Serikali ilitumia jumla shilingi bilioni 10,726.7 chini ya matumizi ya kawaida, ndani ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2014/15; lakini papohapo imeripotiwa idadi hiyo ni shilingi bilioni 11,508.9; rejea maelezo ya Waziri wa Fedha kwa Kamati ya Bunge lote, tarehe 29 Aprili 2015. Tofauti ni shilingi bilioni 782.2
(ii) Kwa kipindi kuanzia Julai 2014 hadi Machi 2015, imeripotiwa shilingi bilioni 526.2 zilitolewa kwa mradi wa BRN, na papohapo imeripotiwa ni shilingi bilioni 526.4; rejea maelezo ya Waziri wa Fedha kwa Kamati ya Bunge tarehe 29 Aprili 2015. Tofauti ya shilingi milioni 400.
f) Deni la Taifa
41. Mheshimiwa Spika, Waziri ameeleza “hadi Machi, 2015, Deni la Taifa likijumuisha deni la ndani na la nje la Serikali pamoja na deni la nje la sekta binafsi lilifikia dola ya Marekani bilioni 19.5 sawa na shilingi trilioni 35 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 18.7 sawa na shilingi trilioni 30.6 Machi 2014, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 21.” Pamoja na kauli ya Waziri kuwa deni la taifa linahimilika, kasi ya kukua kwa deni la taifa linazidi kasi ya kukua kwa pato la taifa. Tuna historia ya kushindwa kulipa madeni na kuomba kufutiwa madeni mwaka 2000 na 2006.
42. Mheshimiwa Spika, kutokana na kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine Duniani, tarehe 11 Juni 2015, siku waziri alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni, thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani ilikuwa ni sawa na sh. 2066 kwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania. Hivyo, deni halisi la Tanzania kwa sasa ni shilingi trilioni 40.287. Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2014, kinakadiria idadi ya Wanzania ni milioni 46.1. Kwa takwimu hizi ni kwamba kila Mtanzania anadaiwa wastani wa Shilingi 873,904. 56.
g) Bei ya Mafuta
43. Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza kurekebisha sheria ya mafuta ya petrol, SURA 392 kwa kuongeza kodi kwenye mafuta ya dizeli na petroli kwa asilimia 100% (kutoka Sh. 50/ hadi Sh. 100/ kwa lita) na asilimia 150% kwa mafuta ya taa (kutoka Sh. 50/ hadi Sh.150/ kwa lita). Sababu kubwa inayotolewa na Waziri wa Fedha ni kwamba ongezeko la kodi kwenye mafuta ya taa ni kuondoa uwezekano wa uchakachuaji wa mafuta. Sidhani kama hii inaingia akilini kwa watendaji na wasimamizi wa serikali kwa kushindwa kwao kudhibiti uhalifu wa namna hiyo kutaondoa uwezekano wa uchakachuaji. NI dhahiri kuwa ongezeo la gharama ya mafuta ya taa, ndio kutakapochochea uchakachuaji wa ubora wa mafuta ya taa badala ya upunguza.
44. Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba kwa serikali kuongeza kodi kwenye mafuta hakuna dhamira njema kwa wananchi wa Tanzania na kwamba kutaongeza zaidi bei ya uzalishaji na usafirishaji jambo ambalo litasababisha ongezeko la bidhaa na huduma. Ongezeko la bei ya mafuta ni suala mtambuka litakasababisha mfumuko mkubwa wa bei na hatimaye kuongeza uchungu na ugumu wa maisha ya mtanzania kwa sababu bei za usafiri na bidhaa za mazao zinazosafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine pia zitapanda. KUB inauliza inakuwaje udhaifu wa Serikali katika kudhibiti ubora wa mafuta iwe ni janga kwa watanzania na hasa wale wa kipato cha chini?
h) Pensheni kwa Wastaafu
45. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikicheza na akili za watanzania kwa kutaja tarakimu za kifedha bila kuzingatia uhalisia na dhamira inayoweza kuleta ustawi wa maisha ya watu hususan wastaafu. Serikali imeongeza pensheni ya kima cha chini kwa kiasi cha shilingi 35,000 kwa mwezi kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 85,000 na kujigamba kwamba imeongeza asilimia 70. Je, ni kwa kiasi gani kiasi hicho cha shilingi 35,000 ambacho kikigawanywa kwa siku ni sawa na shilingi 2,833.33 kinaweza kumfanya mstaafu aishi kwa siku moja. Labda niulieze swali, katika wizara ya Fedha ni nani kati yenu anaweza kujikimu kwa shilingi 2800 kwa siku? Je waziri anaweza? Manaibu wake wanaweza? Wabunge wenzangu mnaweza? Je, huku ni kutenda haki kwa wazee wetu waliotumikia Taifa letu kwa uadilifu na uzalendo mkubwa?
IV. BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KWA MWAKA WA 2015/2016.
46. Mheshimiwa Spika, bajeti mbadala ya KRUB, ni tulivu na yenye kuleta matumaini yenye heri kwa Watanzania. Katika kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2014, Juni 2015 kilichotolewa na wizara ya fedha ukurasa wa (xix) kinaonesha takwimu za awali za Pato la Taifa kwa mwaka 2014 ni shilingi milioni 79,442,499 . Kwa kutumia takwimu za wizara ya Fedha za sasa kutoka kwenye hotuba ya waziri, ya tarehe 11 Juni 2015 , baada ya kufanya uchambuzi wa kihisabati; Pato la Taifa kwa sasa ni shilingi trilioni 94.2 . Angalia jedwali la II;
Jedwali II
Shilingi Asilimia
Mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya Pato la Taifa 13,475,644,000,000 14.3
Pato la Taifa 94,235,272,727,272 100
47. Mheshimiwa Spika, aidha hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015, aya ya 104 ukurasa wa wa 59, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa asilimia 19.2 ya Pato la Taifa. Takwimu za Hali ya Uchumi mwaka 2014, zinaonesha Pato la Taifa limeongezeka kwa asilimia 12.
48. Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio wazi kwamba; tukiweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipa kodi, tukipanua wigo wa kodi, tukiwa na sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, ufanisi ukiongezeka TRA kwa asilimia 50, kudhibiti ukwepji wa kodi, kupunguza misamaha isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa, kuongeza ufanisi bandari ya Dar-es Salaam, kuweka mazingira mazuri na endelevu sekta ya Utali, kukusanya kwa ufanisi mapato kwenye sekta za uvuvi, maliasili, nyumba,ardhi n.k. Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hadi kufikia aslimia 20 mpaka 25.
49. Mheshimiwa Spika, washindani wetu wakubwa katika ukanda huu wa Afrka Mashariki wameshafikia ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 22 ya Pato la Taifa, na hawana maingira mazuri ya uwekezaji na raslimali nyingi kama Tanzania.
50. Mheshimwa Spika, inawezekana kutekeleza kwa vitendo aya ya 48 hapo juu. Hivyo, KRUB inapendekeza kukusanya shilingi bilioni 19,695.2 ambapo mapato ya kodi na yasiyo ya kodi shilingi bilioni 18,847.1 sawa na asilimia 20 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato ya Halmashauri ni asilimia 0.9 ya pato la Taifa sawa na shilingi bilioni 848.1
V: SURA YA BAJETI MBADALA MWAKA 2015/2016
Jedwali III
MAELEZO MAPATO KATIKA SHILINGI (TZ)
A Mapato ya ndani ya Kodi na yasiyo ya kodi 18,847,054,545,454.00
B Mapato ya Halmashauri 848,117,454,545.45
JUMLA MAPATO YA NDANI 19,695,171,999,999.45
C Mikopo na misaada ya Kibajeti 660,337,000,000.00
D Mikopo na Misaada ya miradi ya maendeleo ikijumuisha MCA (T) 1,662,181,000,000.00
JUMLA YA MIKOPO NA MISAADA YA NJE 2,322,518,000,000.00
JUMLA YA MAPATO YOTE 22,017,689,999,999.45
MATUMIZI 15,998,760,300,000.00
E Matumizi ya Kawaida
(i). Mfuko mkuu wa Serikali 1,948,551,500,000.00
(ii).Deni miradi ya maendeleo 2,499,499,000,000.00 .
(iii).Mishahara 7,113,129,100,000.00.
(iv).Wazee 1,200,000,000,000.00
Wizara 2,674,372,000,000.00
Mikoa 34,445,700,000.00
Mamlaka ya Serikali za Mitaa 528,763,000,000.00
H Matumizi ya Maendeleo 6,018,929,699,999.45
Kukuza Uchumi Vijijini (35%) 2,106,625,394,999.81
Huduma za Jamii (28%) 1,685,300,315,999.85
Miundombinu (17%) 1,023,218,048,999.91
Usimamizi wa Ardhi (12%) 722,271,563,999.93
Michezo na Sanaa (8%) 481,514,375,999.96
JUMLA YA MATUMIZI YOTE 22,017,689,999,999.45
VI: ULINGANISHO KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA KWA MWAKA 2015/2016
Jedwali IV
BAJETI MBADALA YA KAMBI YA UPINZANI 2015/2016 BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2015/2016
1 Bajeti isiyo na Mikopo ya kibiashara hivyo bajeti inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni. Bajeti ya Serikali ina mikopo yenye masharti ya kibiashara ya 10% na hivyo bajeti hii inawaongezea wananchi mzigo wa madeni.
2 Bajeti inayoendelea kusisitiza umuhimu wa kuwalipa pensheni wazee wote nchini wenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Bajeti ya Serikali iko kimya kabisa kuhusu malipo ya pensheni kwa wazee wote nchini. Kwani bado inaendelea kufanya upembuzi yakinifu usioisha.
3 Bajeti inayoendelea kusisitiza kushusha kiwango cha tozo ya kodi ya mapato ya ajira kwa wafanyakazi (PAYE) hadi kufikia asilimia 9. Bajeti ya Serikali imeendelea kuwakandamiza wafanyakazi kwa kutoza asilimia 11 ya kodi ya mapato ya ajira (PAYE) kwa wafanyakazi
4 Bajeti ya Upinzani imeainisha vyanzo vipya vya mapato ya ndani na hivyo inayojitegemea kwa asilimia 89.5 Bajeti ya Serikali ni tegemezi kwa asilimia 10.32 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa na hivyo kuongeza deni la taifa.
5 Bajeti Mbadala, mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi ni asilimia 20 ya pato la Taifa Bajeti ya Serikali, mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi ni asilimia 14.3 ya pato la taifa.
6 Bajeti inayolenga kupunguza misamaha ya Kodi hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa ili kuongeza mapato ya ndani. Bajeti ya Serikali imetaja tu azma ya kupunguza misamaha ya kodi bila kufafanua kwa undani
7 Bajeti inayolenga kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo kwa kutenga asilimia 27.34 ya bajeti yote kugharamia miradi ya maendeleo. Bila kukopa katika mabenki ya ndani Asilimia 26.31 ni matumizi ya Maendeleo. Hii ni pamoja na kukopa kibiashara katika mabenki ya ndani
8 Bajeti inayolenga kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo ambavyo havimuumizi mwananchi wa kawaida Bajeti ya Serikali imelenga kukusanya mapato kutoka katika bidhaa zinazotumiwa kila siku na wananchi hivyo kuongeza ugumu wa maisha.
9 Matumizi ya Kawaida ni asilimia 72.66 ya bajeti yote baada ya kutenga fedha za wazee na kuongeza mishahara kwa 10% Matumizi ya Kawaida ni 73.69
10 Bajeti ya kumsaidia mwananchi wa kawaida kutoka katika wimbi la umaskini. Bajeti isiyo mtambua mwananchi maskini na kuongeza matumizi makubwa kwa watawala.
VII: HITIMISHO
51. Mheshimiwa Spika, Rais wa Marekani, hayati Abraham Lincoln aliwahi Kusema; “unaweza kuwadanganya baadhi ya watu wakati wote. Unaweza kuwadanganya watu wote kwa wakati fulani lakini huwezi kuwadanganya watu wote wakati wote”. Naye mwanamapinduzi wa Kisoshalisti, V.I. Lenin anakita kwa kusema; “ukweli ni thabiti”. Serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere iliyowakilisha uzalendo, uadilifu, uwazi, umoja, ushupavu, matumaini na matarajio, sio tu kwa Watanzania, Afrika na Waafrika, bali pia kwa wanyonge wote wa dunia hii wanaoonewa na kunyanyaswa. Tanzania ilikuwa Paradiso, kitovu cha fikra na harakati za ukombozi barani Afrika na Dunia ya Tatu kwa ujumla.
52. Mheshimiwa Spika, Leo hii linapozuka wimbi la viongozi wa Serikali iiyopo madaraani na wa Chama kinachoongoza Serikali na kuinyoshea kidole Serikali juu ya rushwa na ufisadi, unaozidi kutamalaki ni kilelezo tosha kwamba Paradiso imepotea. Aidha, Serikali ya CCM imeendelea kutetea maovu hata yaliyo wazi. Inaendelea kuwabeba wasiobebeka na kuwasafisha wasiosafishika. Hii inamaana kuwa ustahimilivu wa watanzania unatumika kwa hadaa na dharau.
53. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa njia mojawapo sahihi na ya kidemokrasia ni kufanya uchaguzi kwa njia ya sanduku la kura. Nawaomba Watanzania wote wenye umri wa kupiga kura mwezi Oktoba wajiandikishe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa wingi, ili waweze kutumia haki yao ya kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi watakao watumikia kwa kipindi cha miaka mitano, wenye sifa kuu nne; wenye uwezo, wenye kumcha Mungu, wenye kusema ukweli na waochukia ufisadi na maovu mengine yote katika jamii.
54. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi minne ijayo kuanzia sasa , Serikali ya CCM ianze kujiandaa kisaikolojia kuondoka madarakani na kupiisha kwa Amani Serikali adilifu itakayoongozwa na UKAWA kuingia madarakani ili waweze kuwatumikia Watanzania. Aidha, ninawasihi wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi watende haki. Kwa kuwa Amani ni Tunda la Haki.
55. Mheshimiwa Spika, kwa kipekee napenda kuwatakia ndugu zangu waislamu maandalizi ya mfungo wa Ramadhan, na kuwaomba katika mfungo huu, watumie nafasi hii kuiweka Tanzania katika dua zao. Ramadhan Kareem. Na wale wote mtakaoshiriki katika uchaguzi Mkuu, ninawatakia muwe na utulivu wa ndani na uchaguzi wenye Heri, Amani na Utulivu. Ndimi zetu na matendo yetu yatanguliwe na masilahi mapana ya Mama Tanzania. Kwani, matendo yetu mema tukiwa hapa duniani ni sauti huru na hai wakati miili yetu itakapokuwa makaburini.
56. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.
James Francis Mbatia (Mb),
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni –Wizara Ya Fedha
15.06.2015
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni –Wizara Ya Fedha
15.06.2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni