Msajili wa vyama aonya matumizi makubwa kampeni za uchagu
Msajili wa vyama vya siasa nchini JAJI FRANCIS MUTUNGI
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa tahadhari kwa wagombea
watakaokiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 watakuwa
wanajiweka katika hatari ya kutoteuliwa na vyama vyao.
Hadi sasa vyama ambavyo makada wake wameanza kuchukua fomu za kuomba
kuwania urais ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (pichani), alitoa
tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi na sheria ya vyama vya
siasa ambazo zinapaswa kuzingatiwa na vyama na wanasiasa katika kipindi
hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
“Natoa tahadhari au angalizo kwa vyama vya siasa na wanasiasa wasipuuzie
utii wa sheria ya gharama za uchaguzi kwa sababu kutawaathiri nje na
ndani ya vyama ,” alisema.
Mutungi alisema katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mgombea yeyote
au chama cha siasa asipozingatia sheria hiyo atakuwa anahatarisha
nafasi yake ya kugombea na kutoteuliwa na chama chake kutokana na
kukiuka masharti yaliyopo ndani ya sheria hiyo.
Alisema chama cha siasa kitakachopuuzia sheria ya uchaguzi na
kikapitisha mgombea ambaye amekiuka masharti yaliyomo ndani ya sheria
hiyo kitakuwa kinapitisha mgombea ambaye atawekewa pingamizi na atakuwa
amejiharibia nafasi hiyo.
“Sitaki kuamini kuwa sekretarieti ya chama kilichosajiliwa kisizingatie
utii wa sheria ya uchaguzi, kila mtu ni jukumu lake kuzingatia utii wa
sehria bila shututi,” alisema.
Jaji Mutungi alisema kipindi hiki siyo muda mwafaka wa kufanya tathmini
kama vyama vya siasa na wagombea wamezingatia sheria hiyo kwani hivi
sasa ofisi ya msajili na vyombo vingine vinaendelea kufuatilia suala
hilo na muda ukifika matokeo yatatolewa kwa kuweka wazi vyama na
wagombea waliokiuka sheria.
Aliongeza kuwa sheria ya gharama za uchaguzi madhumuni yake yaliwekwa
kwa misingi ya kutaka kudhibiti matumizi ya gharama katika mchakato wa
uchaguzi na kuthibiti vitendo vinavyokataza na sheria ya nchi.
“Vyama vya siasa vinapaswa kufahamu kuna mambo ambayo sheria inakataza
ikiwamo kufanya malipo kwa wapigakura ili kumchagua mgombea fulani,
kuahidi kazi ama cheo, kutoa mikopo na ahadi ama makubaliano yoyote kwa
mpiga kura ili kumchagua mgombea,” alisema.
Sheria ya gharama za uchaguzi imeainisha wazi kuwa chama cha siasa
ndicho kitagharamia mchakato wa kura ya maoni na kampeni za uchaguzi
ikiwa ni pamoja na gharama zote zitakazotumika kwa ajili ya
uhamasisahaji kwa lengo la kumnadi mgombea kwa wapiga kura.
Pia sheria hiyo inaelekeza kuwapo kwa uwazi katika mapato na matumizi ya vyama na wagombea wao kabla na baada ya uchaguzi.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari 2010.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni