Lebo

Jumatano, 17 Juni 2015

Wana-CHADEMA wagoma kuruhusu Mhe.Freeman Mbowe kufungwa jela mwaka mmoja

Mhe.Freeman Mbowe akiwahutubia wananchi katika moja ya mikutano yake


Mahakama wilayani Hai imemtaka Mbunge wa jimbo hilo ambae ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Mhe. Freeman Mbowe kulipa faini ya millioni Moja kama faini kwa kosa la jinai lililokuwa likimkabili.
Faini hiyo imetolewa licha ya upande wa mashitaki kukosa shahidi hata mmoja kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo tangu ilipofunguliwa mwaka 2010 mshitaki ambaye ni mtoto wa mwenyekiti wa mtaa akidai kupigwa na Mhe.Mbowe baada ya kukutwa akipiga kampeni siku ya uchaguzi.
Kesi hiyo iliyodumu kwa miaka mitano ilipata kulalamikiwa mara nyingi na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba haina mashiko na mahakama ilikuwa ikituhumiwa na wafuasi wa CHADEMA kwamba ilikuwa inatekeleza njama za kumchafua Mhe.Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho vile vile ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Kufuatia hukumu hiyo, nimepata kuongea na Mwenyekiti wa Baraza la Maendeleo ya Vijana (BAVICHA) ambaye pia ni mtaalamu wa sheria Kamanda Patrobass Katambi amesema, "Kimsingi haki ya mtu haiwezi kupotea labda kucheleweshwa tu, ni dhahiri kesi kama hizi zilikuwa zinampotezea muda Mwenyekiti wetu Mhe.Freeman Mbowe lakini sasa atakuwa huru zaidi. Kwa hiyo kwa ufupi hizo ndizo changamoto za kisiasa katika hizi nchi zetu lakini ni lazima tusimame imara kwa manufaa ya wanyonge".
Kuhusu mwitikio wa wananchi katika kesi hiyo Kamanda Patrobass amesema, "Inatia moyo kuona wananchi wanawatetea viongozi wao wa CHADEMA, wanajua kwamba wanawapigania na wanashitakiwa kwa hila, ndiyo maana mahakama ilipotoa hukumu tu basi wananchi wamejichangisha shilingi milioni moja ili kulipa fidia na hatimaye wameondoka eneo la mahakama wakiwa na furaha tele huku wakimsindikiza kiongozi wao kabla hajaanza safari rasmi kurudi Dar es salaam"
Jitihada za kumtafuta mwanasheria wa CHADEMA Mhe.Tundu Antipas Lissu ili atupe ufafanuzi kuhusu muktadha wa kesi iliyokosa shahidi kwa miaka mitano lakini bado ikatolewa hukumu hazikufanikiwa. 
Pamoja na mambo mengine, wafuasi wa CHADEMA wilayani hai wameapa kutokuruhusu viongozi wao kupata tabu pasipokuwa na sababu za msingi. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni