Atangaza nia na kusema haamini majigambo, Ataendeleza yaliyoachwa na Awamu ya Nne.
Mhe.Mizengo Kayanza Peter Pinda |
Pinda maarufu kama "mtoto wa mkulima" alisema hawezi kusema
atafanya nini bali atakachokiangalia ni ilani ya CCM, na hataanzisha
jambo jipya bali kuendeleza pale serikali ya awamu ya nne ilipoishia.
Akitangaza nia baada ya kuchukua fomu katika ofisi za Makao Mkuu ya
CCM, mjini Dodoma, alisema anafanya mambo kimya kimya na hatangazi kama
wengine wanavyofanya na kwamba kwa upande wa miundombinu ambayo
inafanya vizuri ni kwa sababu yeye ni kiranja wa mawaziri husika.
Kaulimbiu yake ni "Wanyonge sasa tuwainue" na kusisitiza amesema
hivyo kwa kuwa mpango wa pili wa maendeleo utayagusa makundi hayo.
“Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, nimesema hivi makusudi, mimi ndiyo
nipo serikalini hivi sasa, kama ni uchungu wa mwana mimi naujua zaidi,”
alisema.
ILANI YA CCM
Pinda ambaye alijitapa kuwa ni mtoto wa serikali za mitaa, alisema
CCM ina utaratibu mzuri kwani hakuna anayeweza kusimama na kusema lolote
bali wanaongozwa na Ilani na kwamba haijatoka hivyo hawezi kusema
atakayofanya.
“Ndani ya Ilani kuna maelekezo yote, sera, mikakati na maelekezo
ikiwamo kuahidi Watanzania nini atawafanyia kwa miaka mitano, kwa sababu
haijatoka sina la kusema, nachoweza kuahidi ikikamilika na kupitishwa
na mkutano mkuu na Mungu kunitambua, sitashindwa kutekeleza ilani hata
kidogo,” alibainisha.
“Nalisema kwa kujiamini kwani nimekuwapo serikanili kwa muda
mrefu, nimefanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi kwa
miaka kumi, Benjamini Mkapa kama Naibu Waziri na sasa nipo na Jakaya
Kikwete kwa miaka nane, hawa pia ni viongozi wa chama hiki na
wanasimamia ilani itekelezwe, nimejifunza mengi, pia mimi ndiyo
msimamizi wa ilani.”
Alisema mambo makubwa ni usimamizi ni uwajibikaji, kupambana na rushwa, kilimo.
DIRA YA MAENDELEO
Alisema katika utelekezaji wa Ilani ya chama chake ni lazima kutelekeza Dira ya Maendeleo ya 2000 -2025, mwaka 2005.
Pinda ambaye ametajwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa muda mrefu,
alisema Rais Kikwete alionekana kuongeza nguvu kwenye eneo hilo, na
Kikwete alianzisha Mpango wa Maendeleo ili kuitekeleza Dira ipasavyo
ambayo inataka ikifika mwisho Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati.
Alisema ndani ya Dira siyo rahisi kuona mambo yote kwa kuwa ni sera
ya jumla na ndipo ulipozaliwa mpango wa maendeleo uliogawanyika katika
miaka mitano mitano, na wa kwanza utakamilika mwaka huu.
NINI KIMEFANYIKA
Alisema ndani ya miaka mitano ilikuwa ya kufufua na kujenga mambo muhimu ambayo ni miundombinu ya barabara, reli na bandari.
“Mkapa alianza Kikwete akaendeleza ndani kuna program ya ujenzi wa
barabara inayotakiwa kumalizika 2018, kuwe na mtandao wa barabra nchi
nzima kuunganisha makao makuu ya kila mkoa kwa barabara za lami.”
“Anachokifanya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ni utekelezaji
wa mpango wa miaka mitano na jingine ni mkakati wa kupunguza umaskini ni
program ndani ya mpango na hivi karibuni wataanza kuandaa mpango wa
pili wa maendeleo wa miaka mitano utalipeleka taifa hadi 2021 ili
ikifika 2025/26 ili kutekeleza Dira.”
Alisema kinachotarajiwa kufanyika kwa miaka mitano ijayo ni kujenga
uwezo wa kiuchumi kwa kujenga viwanda na msisitizo ni viwanda vya
usindikaji wa mazao yanayotokana na wakulima, wafugaji na wavuvi.
MAADUI
Alisema maadui wakubwa wakati wa Mwalimu Nyerere ni umaskini,
ujinga na maradhi, lakini kwa marais watatu waliopita walibainisha
maadui wakubwa wengine uharibifu wa mazingira na utawala bora.
Alisema uchumi imara utawezesha kumaliza maadui ujinga, maradhi na
umaskini, huku uharibifu wa mazingira utafanikiwa kwa kuelimisha umma
kwa kujenga fikra mpya namna ya kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji.
UTAWALA BORA
Alisema unawataka Watanzania wote kutambua tuna wajibu kuhakikisha
nchi iendeshe mambo yake kwa uwazi, viongozi waadilifu watakaolivusha
taifa, kiongozi ambaye kila akikaa anajua watu wake ni maskini anatakiwa
kuwainua. “Wanatueleza mmnefanya vizuri lakini umaskini umepungua kwa
kiasi kidogo sana asilimia 28, tunataka mshuke zaidi…wanasema tatizo
lenu ukuaji wa uchumi umetegemea sekta ya ujenzi, maliasili, uchukuzi,
mchango wake ni mkubwa lakini haugusi jamii kubwa moja kwa moja.”
Alisema wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kupeleka jitihada hizo
kwa wakulima, wavuvi na wafugaji kwa kutumia malighafi kutoka kwa
makundi hayo na hivyo kupunguza umaskini kwa kasi kubwa.
KILIMO
Alisema kinachokimbiza watu kwenye kilimo ni jembe la mkono na
kinachotakiwa ni vifaa vya kisasa, na hivyo ndani ya miaka mitano ijayo
hali za maisha ya watu wa chini zitainuka.
“Kama Mwenyezi Mungu itampendeza nikawa mmoja wa waliochaguliwa, ni
eneo piga geuza, kufa na kupona nitalisimamia kwa nguvu zangu zote,”
alisisitiza na kuongeza:
“Wapo ambao hawataki kusikia hata na kusema ni mambo ya Kikwete,
kinachotakiwa ni kuyabeba na kuyasukuma kwa kuwa msingi upo, tukienda
hivi ndani ya miaka kumi Tanzania itabadilika.”
Aidha, aliwataka viongozi na Watanzania kutobeza juhudi za Kikwete.
RUSHWA
Pinda ambaye pia ni Mbunge wa Katavi, alisema lazima serikali
izingatie utawala bora kwa kupambana na rushwa na uovu wowote wenye
kulirudisha nyuma taifa kimaendeleo.
SERIKALI ZA MITAA
Alisema amekuwapo serikali za mitaa tangu aingie serikalini na
kwamba hati chafu zimepungua kutokana na usimamizi wa karibu alioufanya.
Alisema yeye (Pinda) ndiye mtu sahihi kwani mtu mpya atahitaji muda
wa kujifunza, kuelewa na kuuliza na wakati mwingine ataboronga.
MASHANGINGI
Pinda alisema serikali imepunguza magari ya kifahari aina ya VX8,
ambayo gari moja ni zaidi ya Sh milioni 300, ambayo inawezesha
upatikanaji wa magari mawili au matatu.
Waziri Mkuu aliambatana na wabunge na viongozi wengine ambao ni Dk.
Cyril Chami, Martha Mlata, Dk. Orudencia Kikwembe, Dk. Peter Kafumu,
Meya wa Jiji la dar es Salaam, Didas Masaburi, aliyewahi kuwa mbunge,
Dk. Christan Mzindakaya, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi,
Berbadetta Kinabo.
SOURCE-NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni