Lebo

Alhamisi, 25 Juni 2015

Tofauti ya Muswada wa Sheria ya Fedha 2015 na miswada ya fedha miaka iliyopita

 
Kwa ufupi mswada huu  wa Sheria mpya ya kodi itakayoanza tarehe 1 mwezi ujao itafanya yafuatayo.

1. Itaondoa misamaha ya kodi kwenye maduka ya kijeshi. Kama ulikua umezoea kwenda kunywa bar za jeshi kwa bei ya chini mwezi huu ndio mwisho.

Pia kuondoa misamaha ya kodi kwenye vitu vyote vinavyouzwa jeshini, bei ya maduka ya kijeshi itakua sawa na maduka ya mtaani. Kama unataka kununua vitu jeshini wahi mwezi huu ndio mwisho.

2. Kuondoa misamaha ya kodi kwenye taasisi za dini, wachungaji waliokua wamezoea kuagiza magari ya kifahari kwa bei isiyo na kodi mwezi huu ndio mwisho hivyo kama wameagiza wafanye hima.

3. Kuondoa uwezo wa waziri kusamehe kodi, kipengele cha zamani kilichompa waziri wa fedha kusamehe kodi kinaondolewa, ataruhusiwa tu pale kutakapokua na majanga ya asili kwenye misaada inayoenda huko.

4. Itaondoa misamaha ya kodi kwenye migodi ya dhahabu na madini mengine kwa ujumla.

5. Itawataka watu wote wanaotoza adhabu kama trafic kuchukua mashine za EFD na taasisi zote za kiserikali kutumia hizo mashine.

6. Itaondoa misamaha ya kodi kwa taasisi za serikali zinazofanya biashara zipambane na taasisi binafsi ili kuleta ushindani. Hapo TBC ikae chonjo kupambana katika soko.

Sheria hii mpya ya kodi itaongeza vyanzo vya kodi na kupanua wigo wa kodi. Jisomee mwenyewe hapa chini;



Muswada unapendekeza kutungwa kwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2015. Muswada unaweka masharti kuhusu marekebisho ya sheria mbalimbali kwa lengo la kuweka, kutoza au kubadilisha baadhi ya kodi, tozo au ada. vilevile, Muswada unapendekeza kurekebisha sheria nyingine zinazohusu ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya umma.

Muswada huu umegawanyika katika Sehemu Kumi na Sita. Sehemu ya Kwanza ya Muswada inaainisha masharti ya Utangulizi.

Sehemu ya Pili ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197. Kifungu cha 36 kinarekebishwa ili kuiwezesha Serikali kukopa moja ya nane ya mapato yake ya mwaka kwa mwaka uliopita badala ya wastani wa mapato ya miaka mitatu ya nyuma. Marekebisho hayo yanakusudia kuiwezesha Serikali kukopa fedha nyingi zaidi ikilinganishwa na kiasi cha kiasi cha fedha kilichopokelewa kwa moja ya nane ya mapato yake ya mwaka.

Sehemu ya Tatu inapendekeza kufanya Marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mauzo ya Nje, Sura ya 196. Marekebisho hayo yanakusudia kuongeza kiwango cha kodi ya mauzo nje ya nchi cha ngozi ghafi kutoka asilimia sitini ya thamani ya bidhaa (F.O.B) hadi asilimia nane au 0.52 ya Dola za Marekani kwa kilo moja, au yoyote iliyo ya zaidi. Asilimia hiyo itakuwa ni sawa na shilingi za kitanzania mia sita kwa kilo. Sehemu hii pia inapendekeza kuanzisha kodi ya mauzo nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia tano ya thamani ya bidhaa kwa ngozi mbichi ya bluu (wet blue leather) (F.O.B.).

Marekebisho haya yanalenga kupambana na uingizaji wa ngozi mbichi kinyume na sheria na kuwianisha viwango kuwa sawa na zile za nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sehemu ya Nne ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41. Kwa kufanya hivyo, inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 20 kwa lengo la kuwianisha kiwango cha uwekezaji kwa miradi ya michezo ya Bahati Nasibu ya Taifa na muda wa leseni.

Sehemu hii pia inapendekeza kurekebisha kifungu cha 26 ili kuongeza mapato ya Serikali kwa kuanzisha leseni kuu (principal licence) ya michezo ya mashine za kamari (ambayo pia inatozwa kodi) na kuanzisha “hati inayofaa” (certificate of suitability) na kodi ya vifaa vya michezo ya kubahatisha.

Aidha, Sehemu hii pia inapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 31A kwa madhumuni ya kuanzisha kodi ya ushindi kwa kiwango cha asilimia kumi na nane. Lengo la marekebisho haya ni kupanua wigo wa kiwango cha kodi kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.

Halikadhalika, Sehemu hii inapendekeza kurekebisha vifungu vya 41 na 82 kwa lengo la kupunguza migongano baina ya wauza bidhaa mbalimbali zilizoainishwa chini ya Bahati Nasibu ya Taifa, na kusimamia au kudhibiti matumizi ya vifaa vya michezo ya kubahatisha visivyofaa.

Vilevile, inapendekeza kuweka masharti ya adhabu kwa ukiukwaji wa masharti yanayohusu viwango na vifaa vya michezo ya kubahatisha.

Sehemu ya Tano ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332. Kifungu cha 10 kinarekebishwa ili kuweka ukomo wa mamlaka ya Waziri kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa mapato yanayotokana na miradi ya Serikali inayofadhiliwa na mikopo ya kibiashara kwa lengo la kuhakikisha kuwa misamaha ya kodi ya mapato inapunguzwa na hatimaye kupanua wigo wa kodi.

Aidha, inapendekezwa kurekebisha Jedwali la Kwanza na la Pili kwa lengo la kupunguza kodi ya mapato ya ajira (Pay As You Earn) kutoka asilimia kumi na

mbili hadi asilimia kumi na moja na kuweka kiwango cha kodi ya makadirio kwa asilimia ishirini na tano.

Kwa ujumla, Sehemu hii inapendekeza kutoa msamaha wa kodi ya mapato yatokanayo na mauzo ya hatifungani zitakazotolewa na Benki ya Maenedeleo ya Afrika Mashariki katika soko la mitaji la Dar es Salaam. Marekebisho haya yanakusudia kuboresha mapato ya watumishi, kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, kupunguza gharama ya usimamizi wa ukusanyaji kodi, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza makubaliano ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuisaidia Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki.

Sehemu ya Sita inapendekeza kurekebisha Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Sura ya 38. Kifungu cha 20 kinarekebishwa ili kutambua uwekezaji mahsusi kwa lengo la kuweka utaratibu wa kutambua na kutoa hadhi ya uwekezaji mahususi kwa madhumuni ya kutoa na kufuta misamaha ya kodi na kufuta misamaha ya kodi kwenye uwekezaji huo. Aidha inapendekezwa kufuta misamaha ya kodi kwa matela yanayotoka nje ya nchi na kuondoa mabomba aina ya PVC na HDPE yanayotambulika kwenye HS Code 3917.31 yaliyopo katika orodha ya bidhaa za mtaji.

Sehemu ya Saba inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Petroli, Sura ya
392. Kifungu cha 32 kinarekebishwa kwa lengo la kumpa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha kutoa msamaha wa ya petrol kwa mafuta yanayotumika kwenye miradi ya Serikali inayofadhiliwa na wahisani kwa mujibu wa mikataba baina ya Serikali na wahisani.

Sehemu ya Nane ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sura 290. Marekebisho hayo yanalenga kupanua wigo wa kodi kwa kujumlisha ushuru wa hoteli unaokusanywa kutokana na tozo za nyumba za kulala wageni au hoteli na kuanzisha taratibu wa ukusanyaji, ulipaji na usimamizi wa kodi kwa njia ya kielektroniki.

Aidha, Muswada unapendekeza kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya Serikali za Mitaa kuandaa taratibu za kusimamia utekelezaji wa mifumo ya ususanyaji na malipo ya kielekroniki.

Sehemu ya Tisa ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Kodi ya Majengo ya Mamlaka za Miji, Sura 289. Marekebisho haya yanapendekeza kuipa Miji na Wilaya mamlaka ya kutoza kodi ya majengo. Vilevile, inapendekeza kuipa Miji na Wilaya mamlaka ya kutamka maeneo yanayotakiwa kutozwa kodi ya majengo.

Sehemu ya Kumi inapendekeza kurekebisha Sheria ya Reli, Sura 170 ili kuanzisha tozo ya kuendeleza reli ya asilimia 1.5 kwenye thamani ya bidhaa inapofika bandarini (CIF) kwa bidhaa zinazoingia nchini isipokuwa zile zilizosamehewa kodi chini ya Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2004. Mapato yatakayotokana na tozo hii yatatumika kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya reli.

Sehemu ya Kumi na Moja ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263. Marekebisho haya yanalenga kumpa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania mamlaka ya kukusanya michango inayotozwa chini ya Sheria hiyo.

Sehemu ya Kumi na Mbili ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura ya 399. Jedwali la Kwanza la Sheria hiyo linarekebishwa ili kuzijumuisha Sheria ya Reli na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi. Madhumuni ya marekebisho haya ni kutambua mamlaka ya Kamishna Mkuu wa Malaka ya Mapato ya kukusanya tozo na michango kwa niaba ya mamlaka husika.

Sehemu ya Kumi na Tatu inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Elimu na mafunzo ya Ufundi stadi, Sura ya 82. Lengo la marekebisho haya ni kujumuisha wakulima katika Sheria ya Msamaha wa Tozo ya Ufundi stadi ambao wameajiriwa katika mashamba.

Sehemu ya Kumi na Nne inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348. Muswada unapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 11 ili kuzitaka wakala, mashirika ya umma, mamlaka za umma au taasisi za umma zinazotoa au kukusanya ada kwa huduma zinazotoa na kuchangia asilimia kumi na tano ya mapato yake ya jumla kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina kwa kila mwisho wa robo mwaka wa fedha.

Sehemu ya Kumi na Tano ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Barabara, Sura ya 220. marekebisho haya yanalenga kuongeza viwango vya bei ya mafuta ya petrol na dizeli. Bei ya mafuta ya petroli inaongezeka toka shillingi 263 kwa lita hadi shilingi 283; na bei ya mafuta ya dizeli inaongezeka kutoka shilingi 263 hadi shilling 348 kwa lita. Vilevile, inapendekezwa kuwa fedha zitakazopatikana kutokana na ongezeko la bei ya mafuta zitumike kugharamia usambazaji wa umeme vijijini kwa kupitia Mfuko wa Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini (REA).

Sehemu ya Kumi na Sita ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura ya 370. Muswada unapendekeza kurekebisha kifungu cha 8 ili kuwataka wakala mashirika, mamlaka au taasisi za umma, kuchangia asilimia kumi na tano ya mapato ghafi yake kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Kwa sasa, wakala, mashirika, mamlaka na taasisi hizo zinachangia asilimia kumi ya mapato ghafi ya mwaka.

Aidha, Muswada unapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 10A. kwa lengo la kuweka ukomo wa matumizi kwa baadhi ya mashirika na taasisi zinazojiendesha bila ruzuku ya Serikali kwa lengo la kuweka utaratibu utakaosaidia kudhibiti matumizi na kuyawezesha mashirika na taasisi za Serikali kuchangia ipasavyo kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina.

Dar es Salaam, SAADA M. SALUM

11 Juni, 2015 Waziri wa Fedha

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni