Katika kile kinachothibitisha upungufu wa vifaa vya BVR na uchache wa siku za kujiandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais mnamo mwezi oktoba, zoezi hilo limechukua sura mpya mkoani Geita katika kata ya Kalangalala baada ya vijana kuamua kulala vituoni ili kuwahi zamu ya kujiandikisha huku wengine wakinekana na vyandarua mikononi kama anavyoonekana kijana mmoja hapo pichani.
Hatua hizo zimechukuliwa baada ya kushuhudia na wengine kupata habari kwamba watu wengi walinyimwa fursa ya kujiandikisha katika kata la Buhalahala baada ya waatendaji wa tume kuondoka na vifaa hali watu wengi wangali bado hawajiandikisha na wengi wakiwa katika foleni. Hatua hii imepelekea watu wengi kumiminika maeneo ya Kalangalala ili wapate fursa ya kujiandikisha ugenini hali wenyeji wakinyimwa fursa hiyo au wakiipata kwa kulala vituoni.
Katika kituo cha shule ya msingi za Mkoani, kumekuwa na idadi kubwa ya wananchi huku mashaka makubwa yakiwa ni kama watajiandikisha ndani ya muda muafaka au lah. Katika kituo cha Nyanza, kuna idadi kubwa ya wakazi huku kukiwa malalamiko juu ya urasimu katika zoezi hilo, hii ni baada ya watu kuandika majina maalumu kwa lengo la kujiandikisha lakini majina hayo yamepotea katika mazingira ya kutatanisha hivyo kupelekea usumbufu mkubwa.
Kwa upande wa kina mama wajawazito, walemavu na wazee hali imekuwa mbaya zaidi kwani hupewa fursa ya kujiandikisha kwa wakati maalumu huku wengine wakikata tamaa ya kujiandikisha na kurudi nyumbani.
Pamoja na changamoto hizo, hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa katika maeneo mengi ya mji wa Geita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni