Lebo

Jumanne, 30 Juni 2015

PIUS MSEKWA: CCM ni chama kilichopoteza umaarufu kutokana na kashfa za ufisadi

Image result for kinana ccm
KATIBU MKUU WA CCM


 
MHE.PIUS MSEKWA
Wakati ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijiandaa kikamilifu katika hatua za awali za uteuzi wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwanachama mkongwe na aliyepata kuwa spika wa bunge la jamhuri kwa kipindi kirefu Mhe.Pius Msekwa ameyatoa ya moyoni mwake akielezea mwenendo mbaya wa chama chake katika ngazi tofauti.
Akizungumza na kituo cha redio cha East Africa Redio mapema leo asubuhi, Mhe.Msekwa amesema wananchi wamepoteza imani kwa chama hicho kutokana na kugubikwa na kashfa nyingi za ufisadi mkubwa unaorudisha nyuma maendeleo ya taifa huku viongozi wa chama hicho wakishindwa kuwawajibisha wahusika kiasi cha kuwafanya wananchi waamini kwamba chama kinasimamia misingi ya haki na maadili kwa viongozi.

Mhe.Pius Msekwa ametoa takwimu mbalimbali zinazo akisi kushuka kwa umaarufu wa CCM kuwa ni pamoja na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo CCM kilishinda kwa ushindi wa kishindo mwaka 2005 kwa kupata 80% lakini mwaka 2010 kilipata ushindi wa 61%. Pamoja na mambo mengine kashfa zilizotajwa kuwa chanzo kikubwa cha CCM kuporomoka katika siasa za ushindani wa vyama vingi kwa uchaguzi wa mwaka 2010 ni pamoja na kashfa nzito za EPA na Richmond.
Kashfa ya Richmond ndiyo iliyomwondoa Mhe.Edward Lowassa katika nafasi ya uwaziri mkuu kutokana na kutajwa moja kwa moja kuwa alihusika katika mchakato wa utoaji tenda kwa kampuni hewa ya kufua umeme yaani RICHMOND na kuligharimu taifa hasara ya mamilioni ya shilingi.
Mdadisi wa Masuala ya kisiasa ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya siasa na mahusiano ya kimataifa, Mtaalamu John Nzali anachambua kwamba endapo CCM wasipobadilika katika namna ya kuichukulia gadhabu ya umma dhidi ya ufisadi katika taifa huenda itaporomoka zaidi katika uchaguzi mkuu ujao. Amesema, "Kama CCM watashinda basi ni kwa asilimia si zaidi ya 60 endapo hawatafanya mabadiliko ya namna ya kushughulikia ufisadi, mipango kama KUJIVUA GAMBA haijawa na matokeo chanya mbele ya umma haswa baada ya kuongezeka kwa kashfa nyingine kama vile Tegeta Esrow. Kwa kifupi endapo wapiga kura wataendeleza kadhia ya kuchukia ufisadi na kutumia kura kama fimbo, hii inamaanisha kwamba CCM wanaweza kushuka kwa asilimia nyingine 30 kutoka kwenye 60% za mwaka 2010 endapo UKAWA watamuweka mgombea anaekubalika kwa wananchi vinginevyo mwenyekiti wa chama lazima achukue maamuzi magumu katika kumpata mgombea mwaka huu.
Image result for jakaya kikwete ccm
Mwenyekiti wa CCM, Mhe.Rais Jakaya Mrisho Kikwete
 Kuhusu mahusiano ya Tanzania na mataifa ya nje mathalani nchi wahisani, Ndugu Nzali amesema, "endapo mtu rais ajaye atatokana na chungu cha ufisadi, kama taifa tutakuwa katika wakati mgumu kwani huenda nchi wahisani zikazidi kukaza kamba ya kupunguza misaada kwa kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kila mara ikiwa kama mbinu mojawapo ya kuishinikiza serikali kupambana na ufisadi"
Chama Cha Mapinduzi kinatarajiwa kumpitisha mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho siku chache mbeleni huku kukiwa na ushindani mkali baina ya watangaza nia zaidi ya 40 waliochukuwa fomu za kuomba ridhaa akiwemo mgombea wa darasa la saba kutoka kigoma aliyepewa fomu na CCM licha ya katiba ya nchi kutaja wazi kuwa mgombea kwa nafasi ya urais walau awe na shahada moja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni