HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI OFISI YA RAIS – MAHUSIANO NA URATIBU
HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA OFISI YA RAIS
– MAHUSIANO NA URATIBU, MHE. ESTHER NICHOLAS MATIKO (MB), AKIWASILISHA
BUNGENI MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
Inatolewa chini ya Kanuni ya 105(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013.
___________________________
Inatolewa chini ya Kanuni ya 105(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013.
___________________________
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kwanza, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kujalia afya njema na kunilinda dhidi ya maadui na kunipa nguvu na maarifa ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kisiasa na kijamii. Pili nawapongeza viongozi wote wa UKAWA kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Wapiga kura ili wawe na uwezo wa kuamua ni nani atakayeongoza Dola la Tanzania kwa awamu ya tano.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru wana Mara na hususan wana Tarime kwa imani kubwa waliyo nayo kwangu na ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kazi zangu za kibunge. Aidha, naomba muendelee kuisimamia kauli mbiu yetu isemayo “Tarime yetu Mshikamano kwa wote”. Ninapenda pia kutumia fursa hii kuwaomba mniunge mkono ikiwa chama changu kitaniteua kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo. Kipekee naishukuru famila yangu kwa kuendelea kunipa moyo katika majukumu yangu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii ni awamu ya mwisho ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano 2011/12 – 2015/16, na kwa kuwa maisha ya kikatiba ya bunge hili la kumi yanafikia tamati mwaka huu wa fedha, hii itakuwa ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Rais – Mahusiano na Uratibu. Kwa sababu hiyo, napenda kuchukua pia nafasi hii kuwatakia wabunge wote mema huko uraiani baada ya bunge hili kuvunjwa lakini pia niwatakie watia nia wote watakaogombe nafasi mbalimbali za uongozi kupitia UKAWA ushindi wa kishindo ili Serikali ya awamu ya tano itokane na UKAWA.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba namalizia muda wangu kama waziri Kivuli katika Ofisi ya Rais – Mahusiano na Uratibu, lakini nafarijika sana kwani utumishi wangu ulileta tija katika kuiamsha Serikali kutimiza wajibu wake. Hata hivyo, nasikitika kwamba pamoja na hoja zenye tija na ushauri mzuri tulioipatia Serikali hii, hakukuwa na mabadiliko makubwa yenye tija yaliyofanyika kwa kuwa Serikali hii ya CCM kama kawaida yake iliendelea kubeza na kupuuza mapendekezo mazuri iliyopewa na Kambi ya Upinzani Bungeni kwa sababu tu ya kiburi cha madaraka.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inawasihi wananchi wapime kazi na mchango wa Upinzani kwa Serikali ambao haukufanyiwa kazi kwa mustakabali mwema wa uchumi na maisha ya watanzania kwa jumla. Kwa mfano kwa miaka yote kumi ya utawala wa Serikali hii ya CCM ya awamu ya nne Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitaka Serikali kutekeleza masuala yafuatayo:
i. Kusimamia taasisi za fedha ili kuhakikisha kwamba zinatoa riba nafuu ili wananchi waweze kukopa katika taasisi hizo na hivyo kuweza kuendesha shughuli zao za kiuchumi bila kunyonywa. Msingi wa hoja hii ulitokana na ukweli kwamba Riba katika benki na asasi za fedha imeendelea kuwa juu, na sababu mojawapo ya kiwango cha riba kuwa juu ni Serikali kuwa mmoja wa wakopaji wakubwa katika mabenki na asasi za fedha za hapa nchini. Hali hii imesababisha ushindani usio wa haki baina ya serikali na wananchi wanaokopa katika mabenki hayo na anayeumia kwa hali hii ya ushindani na serikali ni mkopaji mdogo. Ushauri huu umeonekana hauna maana kwa kuwa Serikali imeendelea kuwa mkopaji wa ndani na hivyo riba ziemeendelea kuwa juu na wananchi wemeendelea kuumia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawaomba wananchi wapime jambo hili waone kama Serikali hii ya CCM ina sifa za kuendelea kutawala ikiwa inashindana na wananchi wake kukopa kwenye benki za ndani na hivyo kuwanyima wananchi fursa za kukopa na wanapokopa wanaadhibiwa kwa riba kali kutokana na serikali kuwepo katika ushindani.
ii. Tuliitaka Serikali kuzipunguzia kodi shule binafsi hapa nchini ili shule hizo zipunguze ada ili wananchi waweze kumudu kulipia ada watato wao katika shule hizo ili kuondoa matabaka katika utoaji wa elimu. Msingi wa hoja hii ulikuwa ni malalamiko ya wananchi kwamba shule binafsi ambazo zinasadikiwa kutoa elimu bora zaidi kuliko zile za serikali zinatoza ada kubwa sana kiasi kwamba wananchi wenye uwezo mdogo kifedha hawawezi kuwasomesha watoto wao katika shule hizo. Aidha, utafiti unaonesha kwamba shule hizo zinatoza ada kubwa kutokana na wingi wa kodi zinazolipa: kwa mfano, kodi hizo ni kama vile Corporation tax, Value Added Tax, Skills & Development Levy,Land Rent, Local Government taxes: ( ambazo ni: Property tax, City Service levies na Tax for sign boards), Aidha, kodi nyingine ni Fire brigade Inspection fees na Work permit fees kwa walimu kutoka nje. Ushauri huu nao haujafanyiwa kazi na matokeo yake ada kwa shule binafsi bado ziko juu jambo ambalo limesababisha wananchi wengi kushindwa kuwalipia watoto wao ada katika shule hizo. Hili nalo wananchi watapima kuona kama Serikali hii ya CCM ina nia ya ku- “harmonize” ada kwa shule za binafsi na zile za Serikali ili wanafunzi waweze kupata elimu bila ubaguzi.
iii. Katika Sekta ya Nishati, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliihoji Serikali uhalali wa kufungua Akaunti ya Tegeta ESCROW kwenye mgogoro wa TANESCO na IPTL, na uhalali wa kumlipa wakili mabilioni ya fedha za wananchi katika kesi ya ICSID kuhusu mgogoro huo kama IPTL ilikuwa na haki ya kulipwa capacity charges hizo na TANESCO. Serikali iliendelea kupuuza ushauri wa Kambi ya Upinzani na matokeo yake ni ufisadi wa kutisha wa wizi wa zaidi ya shilingi bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow ambapo Serikali haikuambulia chochote. Itakumbukwa kwamba katika Sakata hilo, Mawaziri wawili, Prof. Sospeter Muhongo – aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Ana Tibaijuka – aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali – Frederick Werema waliachia ngazi. Laiti Seirikali hii ya CCM ingekuwa sikivu kama inavyojinasibu, Taifa lisingepata hasara ya mabilioni ya fedha kwa wizi uliofanyika katika sakata la Escrow. Wananchi watapima kati ya hoja za Upinzani za kulisaidia taifa na mbinu chafu za Serikali ya CCM ya kuwakumbatia mafisadi.
iv. Katika Sekta hiyo hiyo ya Nishati na Madini, tuliishauri Serikali kuhakikisha kuwa gesi asilia iliyogunduliwa Mtwara inachakatwa na kujazwa kwenye mitungi kwa ajili ya matumizi ya majumbani badala ya kutegemea mpango wa TPDC wa kusambaza gesi hiyo kwa njia ya mabomba kama mfumo wa maji ulivyo kwa kuwa njia ya mabomba inaweza kuchukua miaka mingi mpaka wananchi wafaidike na gesi hiyo. Msingi wa hoja hii ilikuwa ni kuwapunguzia wananchi mzigo wa bei kubwa ya gesi inayoingizwa kutoka nje ya nchi.
v. Katika Sekta ya Maji, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, iliitaka Serikali kutekeleza bajeti ya Maendeleo katika Wizara ya Maji ili kukamilisha miradi mingi ya maji ambayo haijakamilika. Msingi wa hoja hii ni kutokana na kasumba mbaya ya Serikali ya kutenga fedha ndogo kwa miradi ya maendeleo na hata zile kidogo zilizoidhinishwa na bunge hazitolewi zote na hazitolewi kwa wakati pia. Matokeo ya kasumba hii mbaya ni kwamba miradi mingi ya maji haijakamilika, na ile michache iliyokamilika haitoi maji kwa ufanisi.
vi. Katika Sekta ya Michezo na Sanaa tuliishauri Serikali hii:
Mosi, kuvirejesha viwanja vyote vya michezo vilivyohodhiwa na Chama cha Mapinduzi kwa Serikali ili viwe mali ya umma kama ambavyo viliwahi kuwa chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Pili, kuviendeleza viwanja hivi kwa kuingia ubia na makampuni makubwa ya uwekezaji ama na nchi wahisani ili kurejesha hadhi ya viwanja vitakavyoendana na mahitaji ya kisasa ya viwango na ubora wa viwanja vya michezo.
Tatu, kuhakikisha kuwa uwanja wa Taifa hautumiki katika michezo ya aina yoyote bila ya mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ili kuzuia ubadhirifu wa mapato katika mechi mbalimbali unaofanywa na watendaji wasio waaminifu.
Mheshimiwa Spika, Mambo yote hayo hayajafanyika.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa pia kwamba kwa miaka yote kumi ya utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne ya CCM, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungen, katika hotuba zake za bajeti mbadala, tuliitaka Serikali kutekeleza masuala yafuatayo:
i. Kupunguza misamaha ya Kodi ili isizidi 1% ya Pato la Taifa.
ii. Kupunguza kodi na tozo kwenye Mafuta ya Petroli na Dizeli ili kupunguza mfumuko wa Bei na ukali wa maisha kwa wananchi. Ukitaka kujua kuwa Serikali hii haina huruma kwa mwananchi masikini, imepandisha kodi na tozo kwa mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa katika bajeti hii kwa kisingizio kwamba fedha itakayopatikana katika tozo hizo itakwenda kwenye mfuko wa usambazaji wa umeme vijijini – REA. Kwa ongezeko hili la kodi kwenye mafuta, ni dhahiri mfumuko wa bei utatokea kwa kuwa lazima gharama za maisha zitapanda. Lakini mbaya zaidi, serikali inajitetea kwamba itapeleka fedha zinazotokana na tozo ya mafuta REA, lakini ukweli ni kwamba fedha haziendi REA. REA wanalalamika kwamba wanashindwa kusambaza umeme vijijini kwa kuwa hawapewi fedha, licha ya kwamba ongezeko la kodi kwenye mafuta ya petroli na dizeli mwaka jana, Serikali ilitumia kisingizio hikihiki kwamba itapeleka fedha hizo REA.
iii. Kufanya Marekebisho makubwa katika mfumo wa malipo Serikalini hususan kuondoa Posho za vikao (sitting allowances) kwa watumishi na viongozi wote wa Umma
iv. Kuelekeza raslimali fedha kwenye maendeleo vijijini hasa kujenga miundombinu kama barabara za vijijini na umeme vijijini.
v. Kuelekeza fedha za kutosha kukarabati Reli ya Kati na kufufua njia za Reli za Tanga, Moshi na Arusha. Pendekezo hili limebaki kama hadithi kwenye vitabu vya riwaya.
vi. Kuongeza wigo wa kutoza tozo la ujuzi (Skills Development Levy) ambapo sasa waajiri wote walipe ikiwemo Serikali na mashirika ya umma. Pia kupunguza tozo hii mpaka 4% ambapo 1/3 itaenda VETA na vyuo vya Ufundi na 2/3 itaenda Bodi ya Mikopo ili kukabili changamoto ya mikopo kwa wanafunzi.
vii. Kushusha kima cha chini cha kodi ya mapato (PAYE) mpaka 9% ili kuwezesha wananchi wa hali ya chini kubaki na fedha za kutumia na kukuza uchumi. Serikali imeendelea kushusha kodi hii lakini haijafikia pendekezo letu la asilimia 9.
viii. Kuongeza mapato ya ndani na kupunguza mikopo ya kibiashara kwa kuhakikisha mapato ya ndani yanafikia 20% ya pato la taifa, kuongeza nguvu za kisheria na udhibiti ili TRA ikusanye mapato zaidi kwenye kampuni za simu na kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi.
ix. Kuliandaa Taifa kumiliki uchumi wa Gesi.
x. Kupunguza /kufuta kodi kwenye bidhaaa za vyakula kwa muda maalum ili kushusha mfumuko wa bei.
xi. Kuweka mfumo mpya wa elimu kwa kushirikisha sekta binafsi katika kutoa elimu kwa ubora zaidi, ikiwemo kuundwa kwa chombo cha Udhibiti wa Elimu na Mafunzo (Tanzania Education and Training Regulatory Authority - TETRA)
xii. Kutoa vipaumbele na unafuu vya kikodi kwa viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za hapa nchini hasa za kilimo na zenye kuongeza ajira kama Korosho, Pamba na Mkonge kwa kufuta Kodi ya ongezeko la thamani (zero rated) kwa Viwanda vinavyozalisha bidhaa kwa malighafi za ndani za mazao ya Pamba, Korosho na Mkonge.
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la mapendekezo haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani lilikuwa ni kuiwezesha Serikali kupata mapato ya kutosha kutoka vyanzo vya ndani ili iweze kuutekeleza Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Aidha, tulishauri pia juu ya namna ya kusimamia sekta mbalimbali ili ziwe na tija kwa faida ya watanzania wote. Jambo linalotia shaka kama Serikali hii iko timamu ni pale ambapo inashauriwa kwa faida yake lakini inakataa kutekeleza kwa hasara yake yenyewe.
Mheshimiwa Spika, masuala tuliyopendekeza ni mengi sana siwezi kuyataja yote hapa lakini itoshe kusema kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake lakini kwa kuwa haikuwa na dhamana ya kukusanya kodi, ushauri huo ulibaki kama ushauri tu kwa hisani ya Serikali kutekeleza au kuacha. Na huu ndio msingi wa kuwataka wananchi wachague madiwani, wabunge na rais kutoka UKAWA ili tuunde Serikali na hivyo kuwa na mamlaka ya kukusanya kodi na kuwahudumia wananchi kuliko usanii huu unaofanywa na Serikali ya CCM.
2. SERIKALI YA CCM ILIVYOSHINDWA KUTEKELEZA ILANI YAKE YA UCHAGUZI KUHUSU MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 19 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 -2015 inasema hivi: “Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 hadi 2020 umeainisha jukumu kubwa la nchi yetu katika kipindi hiki ni kutekeleza lengo la Dira 2025 la kuleta mapinduzi ya uchumi yatakayoitoa nchi kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea. Ili kufikia lengo hili Mwelekeo wa CCM unahimiza Serikali kutekeleza majukumu yafuatayo:-
(a) Kujenga Uchumi wa Kisasa wa Taifa Linalojitegemea, yaani
Modenaizesheni ya uchumi
(b) Kutekeleza Sera ya Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi
(c) Kutekeleza Sera ya Dola Kupanga Mipango na Kusimamia Uchumi
(d) Kuongeza uwezo wa Maarifa (sayansi na teknolojia) katika nchi kwa kutilia mkazo ubora wa Elimu na Raslimali Watu ya Nchi.
(e) Kuweka msingi wa miundombinu ya uchumi wa kisasa kwa kuhakikisha nishati yenye uhakika na uboreshaji wa miundombinu na huduma za kiuchumi kwa jumla.
(f) Kutumia fursa za kijiografia katika kukuza uchumi wa kisasa wa nchi.
(g) Kuhimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya kazi
(h) Kuhakikisha uwiano wa mapato ili kujenga amani katika nchi na utulivu wauchumi na maendeleo
(i) Kuweka methodolojia ya kusimamia utekelezaji wa majukumu haya ilikuhakikisha yanafanikiwa”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka wananchi wapime utekelezaji wa ilani hiyo. Nasema hivyo kwa sababu wakati CCM na serikali yake inawahadaa wananchi kwa ahadi ya uwongo kwamba itajenga Uchumi wa Kisasa wa Taifa Linalojitegemea, yaani Modenaizesheni ya uchumi, tafiti za kiuchumi zinaonyesha kwamba Tanzania imeendelea kuwa na nakisi ya bajeti ya takriban asilimia 40 kwa miaka kumi iliyopita. Sababu kubwa ya nakisi ya bajeti imeelezwa kuwa ni Serikali kushindwa kuainisha vyanzo vya mapato vya ndani na hata vile vichache vilivyoainishwa havikusanyi mapato kwa asilimia 100. Kwa sababu hiyo, Tanzania inatumia zaidi kuliko inavyokusanya, na huo ndio msingi wa kuendelea kuwa tegemezi kwa wahisani kila wakati. Kwa maneno mengine, wananchi watambue kwamba Serikali hii ya CCM imeshindwa kujenga uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea kama inavyojigamba kwa miaka yote 53 ya Uhuru. Na kwa kuwa tumekuwa tukipendekeza vyanzo mbadala vya makusanyo ya ndani na Serikali kuendelea kupuuzia mapendekezo hayo, wakati umefika wananchi waiondoshe CCM madarakani ili Serikali mpya ya UKAWA iendeshe nchi kwa viwango baada ya uchaguzi wa Oktoba, 2015.
Mheshimiwa Spika, Wakati Ilani ya CCM inajinasibu kwamba Serikali ya CCM itatekeleza “Sera ya Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi”, taarifa za Kitabu cha Takwimu Duniani ( World Fact Book) za mwaka 2014 zinaonyesha kwamba asilimia 36 ya idadi ya watanzania wako chini ya mstari wa Umasikini. Kuwa chini ya mstari wa umasikini maana yake ni kwamba wanatumia chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku kwa matumizi ya kawaida..
Mheshimiwa Spika, asilimia 36 ni sawa na watanzania milioni 16 na laki mbili (16,200,000), kwa kuzingatia Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 ambapo idadi ya watanzania ilikuwa takribani watu milioni 45. Idadi hii ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umasikini ni sawa na asilimia 67.5 ya wapiga kura milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa mwaka huu. Ndio maana CCM wameendela kuwa na kasumba mbaya ya kutumia umaskini wa watanzania kama mtaji wao wa kisiasa kwa kuwarubuni wananchi kwa vitu vidogogo kama kanga na chumvi ili kujipatia kura.
Mheshimiwa Spika, hii tabia ya kuutumia umasikini kama kete ya kisiasa itakoma Novemba mwaka huu wakati Serikali mpya ya UKAWA itakapoingia madarakani, na kazi kubwa ya Serikali ya UKAWA itakuwa ni kuliondoa taifa kwenye fedheha hii ya umasikini na utegemezi na kujenga mazingira rafiki ili kila mtanzania anufaike na rasilimali za taifa.
Mheshimiwa Spika, kimsingi Serikali imeshindwa kabisa kutekeleza ibara ya 19 ya iIani ya CCM. Kwa mfano, Serikali imeshindwa kuongeza uwezo wa Maarifa (sayansi na teknolojia) katika nchi kwa kutilia mkazo ubora wa Elimu na Raslimali Watu ya Nchi kama ilani yao inavyosema. Hii ni kwa sababu miaka kumi ya Utawala wa Serikali hii ya awamu ya nne ya CCM ndiyo kipindi ambacho Elimu ya Tanzania imeporomoka kuliko miaka yote katika historia ya Tanzania. Ndio kipindi ambacho tulishuhudia asilimia 65 ya wanafunzi wa kidato cha nne wakipata daraja sifuri mwaka 2012 na ndio kipindi ambacho tulishuhudia wanafunzi wakichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM imeshindwa pia “Kuweka msingi wa miundombinu ya uchumi wa kisasa kwa kuhakikisha nishati yenye uhakika na uboreshaji wa miundombinu na huduma za kiuchumi” kwa jumla kama ilani ya CCM inavyosema. Nasema hivi Kwa sababu Kwa mujibu wa taarifa ya Mkakati wa Taifa wa Mageuzi ya Usambazaji Umme Tanzania 2014 - 2025 ni asilimia 24 tu ya kaya za watanzania bara ambazo zimeunganishiwa umeme tangu Tanzania ipate uhuru wake kutoka kwa wakoloni miaka 53 iliyopita. Kati ya hizo, ni asilimia 7 tu ya kaya hizo zipo vijijini na asilimia 17 zilizobaki ni kaya za mijini. Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba ni wananchi wachache sana wameunganishiwa umeme, bado umeme huo si wa uhakika kwani kila mara tunashuhudia umeme ukitolewa kwa mgawo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa namna gani itakuza uchumi vijijini ikiwa kwa miaka yote 53 ya uhuru imeunganisha umeme vijijini kwa asilimia 7 tu na umeme wenyewe si wa uhakika?
3. UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO 2011/2012 - 2015/2016
Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu katika mwaka wa fedha 2011/2012 lilipokea, kujadili na kupitisha Mpango Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ni sehemu ya Mpango wa Muda Mrefu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
Mheshimiwa Spika, Mpango huo ulipendekeza kwamba Serikali iwe inatenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mpango unasema hivi: nanukuu, “kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, Kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Serikali haijawahi hata mara moja kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuna wakati mwingine haikutenga hata senti moja. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali haikutenga fedha yoyote kutoka katika mapato yake ya ndani kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kugoma kutoa asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo, miradi mingi ya maendeleo haijakamilika licha ya kwamba huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, ukisoma Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/15 katika kiambatanisho II cha Mpango (uk. 86 -104) utaona kwamba miradi mingi iko katika hatua za awali za utekelezaji kama vile kufanya upembuzi yakinifu, kutafuta wakandarasi, kutafuta washauri waelekezi, kufanya thathmini ya mazingira (Environmenta Impact Assessment) n.k.
Mheshimiwa Spika, kwa wastani, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2014/15 haukufikia asilimia 50. Hii inatia shaka kama malengo ya Mpango kwa mwaka wa fedha 2015/16 yatafikiwa ikiwa bajeti ya maendeleo itaendelea kuwa finyu na kutotolewa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kutotekeleza Mpango wa Maendeleo ipasavyo ni uasi wa Serikali dhidi ya uamuzi wa Bunge lakini na pia ni udhaifu mkubwa wa Serikali kuanzisha jambo na kushindwa kulisimamia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwa nini haikutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo?
4. MAFANIKIO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KUPITIA PROGRAMU YA TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA - “BIG RESULTS NOW”
Mheshimiwa Spika, mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) uliletwa hapa Bungeni katika mjadala wa Bajeti wa mwaka 2013/2014 kupitia kitu kilichoitwa Presidential Delivery Bureau. Hata hivyo ukitazama kwa makini malengo ya BRN na Mpango wa Maendeleo wa Taifa yanafanana. Kimsingi BRN imeufunika Mpango wa Maendeleo wa Taifa na badala yake sasa maendeleo yanapimwa na BRN badala ya kuangalia malengo ya Mpango kwa ujumla wake. Hii inaleta mkanganyiko katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na kuwa na mipango miwili tofauti na yenye mazingira tofauti ya kibajeti katika utekelezaji wa miradi.
Mheshimiwa Spika, Licha ya kuwa na mipango miwili ya maendeleo inayoshabihiama malengo yake, lakini upimaji wa mafanikio ya mipango hiyo umekuwa ni wa kibabaishaji. Kwa mfano taarifa ya Tume ya Mipango ya Aprili 2015, kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 inasema kwamba moja ya mafanikio ya BRN katika sekta ya Kilimo ni pamoja na kupatikana kwa hati za mashamba mawili ya Bagamoyo na Mkulazi .
Mheshimiwa Spika, hivi Serikali hii ya CCM iko ‘serious’ kusema kwamba upatikanaji wa hati za mashamba ni mafanikio katika Kilimo?. Wananchi wanakula hati au wanahitaji mazao mengi kutokana na kilimo kilichoboreshwa? Inakuwaje Serikali inachukulia suala la utoaji wa hati kama mafanikio katika kilimo wakatia utoaji wa hati ni jukumu la Serikali kupitia sheria na Wizara ya ardhi? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina mtazamo kwamba kama Serikali itaendelea kupima mafanikio kwa vigezo dhaifu na vya kibabaishaji kama hivi, itakuwa vigumu sana kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Katika sekta hiyo hiyo ya Kilimo, Serikali inasifia mpango wa BRN kwamba umeleta mafanikio katika kilimo kwa kuwa sasa uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka tani 4 hadi tani 4.5 kwa hekta katika skimu za umwagiliaji. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba Serikali inafanya mzaha kama inaweza kujivunia ongezeko la kilogramu 500 sawa na gunia tano za mpunga kwa hekta na kuweka ongezeko hilo katika Kitabu cha Mpango wa Maendeleo wa Taifa kama “Matokeo Makubwa Sasa”.
Mheshimiwa Spika, Katika sekta ya elimu, mafanikio yanayoelezwa ni pamoja na ujenzi wa maabara katika shule za Sekondari za Serikali. Ikumbukwe kwamba Agizo la Rais la kujenga maabara katika shule za sekondari lilikuwa ni agizo la kisiasa na halikuzingatia vipaumbele vya bajeti za Halmashauri husika, jambo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwa watendaji na madiwani katika halmashauri nyingi nchini. Aidha, suala hili limewasumbua sana wananchi ambao kila uchao wamekuwa wakichangishwa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, ujenzi wa Zahanati, na Barabara za Halmashauri. Katika maeneo mengi nchini shule nyingi zilikuwa bado hazijamaliza ujenzi wa madarasa. Lakini kabla hawajamaliza ujenzi wa madarasa tayari wanapewa amri nyingine ya ujenzi wa maabara.
Mheshimiwa Spika, Amri hii ya kujenga maabara bila kutenga bajeti kwa ajili ya kazi hiyo imewasababishia adha kubwa sana wananchi na viongozi wao kwa kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakitoa amri wakamatwe kwa kushindwa kutoa michango ya maabara kwa mfano wakuu wa Wilaya za Rorya na Butiama wamekuwa wakitumia polisi kutekeleza amri ya ujenzi wa maabara jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitafsiri kama uonevu kwa wananchi kwa kuwa kazi hiyo ni jukumu la Serikali ambayo inakusanya kodi kutoka kwa wananchi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imegundua kuwa shule nyingi za Kata ambazo husoma watoto wa maskini wa nchi hii wamebadili matumizi ya madarasa na kuweka miundombinu ya maabara ili kukidhi maagizo ambazo yametolewa kisiasa bila kuzingatia bajeti za shule na Halmshasuri husika. Wakati serikali hii ya CCM ikijigamba hapa Bungeni kuwa wamejenga maabara, ni wazi kuwa hawajajenga maabara bali wametoa maelekezo ya kisiasa ambayo yamekuwa mzigo kwa walimu, wazazi na Halmashauri nchini.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa bajeti ya ujenzi wa maabara haikuwahi kuidhinishwa na bunge hili, na kwa kuwa Serikali imetumia ubabe kuwachangisha wananchi fedha za ujenzi wa maabara hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili kama itaendelea kutumia mabavu hayohayo kuwachangisha wananchi fedha za kununulia vifaa na kemikali katika maabara hizo au imetenga fedha katika bajeti kwa ajili hiyo? Aidha, tunaitaka Serikali kueleza bunge hili inachukua hatua gani juu wa wanafunzi waliokosa madarasa ya kusomea baada ya baadhi ya shule nchini kugeuza vyumba vya madarasa kuwa maabara baada ya kushindwa kujenga maabara mpya kufuatia agizo la Rais la kujenga maabara?
Mheshimiwa Spika, Katika sekta ya nishati, Serikali imesema moja ya mafanikio katika sekta ya nishati kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa sasa ni pamoja na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina mgogoro na mafanikio hayo, ila kuna taarifa kwamba ujenzi huo wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umegubikwa na ufisadi mkubwa ambapo gharama za ujenzi huo zimeongezeka mara mbili kuliko ilivyokuwa imepangwa. Kutokana na hali hiyo, tunaitaka serikali kutoa maelezo juu ya tuhuma hizo kwa kuwa mradi huo umegharimu fedha nyingi za walipa kodi.
Sekta ya Uvuvi
Mhemshimiwa Spika, pamoja na sekta ya uvuvi kutegemewa na watanzania wengi waishio sehemu za mito na maziwa bado serikali inaonekana kutokuonyesha dhamira ya dhati katika kuendeleza sekta hiyo, na hii inajidhihirisha katika hotuba ya waziri mkuu ambayo imeonyesha kuwa mazao ya uvuvi yameongezeka toka tani 341,109 mwaka 2006 hadi kufikia tani 375,158 mwaka 2014. Kwa hesabu za haraka inaonyesha katika miaka 9, ongezeko la mazao ya uvuvi ni tani 34,049 tu.Hii ni aibu kwa serikali ya chama cha mapinduzi kwa kutoonyesha jitihada ya kuongeza kipato cha taifa na kuinua uchumi kupitia sekta hii ya uvuvi.
Mheshimiwa Spika, Inasikitisha kuona matatizo yanayowakabili wavuvi kila mwaka ni yale yale ambayo yanasababishwa na mfumo mbovu wa wizara wa kusimamia shughuli za wavuvi nchini. Ukosefu wa soko la uhakika la mazao ya uvuvi, kushindwa kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya samaki na mazao ya uvuvi. Kushindwa huko kunaashiria kuchoka kwa serikali na kusababisha ukosefu wa mapato na hivyo kuendelea kudidimia kwa pato la taifa.
Mheshimiwa Spika, wavuvi wadogo nchini wameendelea kukabiliwa na wakati mgumu jambo ambalo linakwamisha shughuli zao za uvuvi: Changamoto zinazowakabili ni pamoja na:
i. Usumbufu wa upatikanaji wa leseni kwa wavuvi wadogo na malipo ya leseni ya ukaguzi na usajili wa vyombo vya uvuvi kwa wavuvi wadogo kulipishwa kwa thamani.
ii. Kutokuwa na utaratibu rasmi kwa wavuvi wadogo wenye uwezo wa kununua dhana za uvuvi kutoka nje.
iii. Serikali kuacha jukumu la kuelimisha wavuvi wadogo juu ya sheria za uvuvi na uhifadhi wa mazingira maeneo ya uvuvi.
iv. Kutokuwepo mazingira wezeshi kwa wavuvi wadogo ili kuuza mazao yao ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua mchango wa wavuvi wadogo wadogo kambi ya upinzani inashauri yafuatayo ili kuwezesha kuwa na uvuvi endelevu wenye tija na kuchangia uchumi katika nchi yetu:
i. Serikali iweke mfumo wa uwazi wa upatikanaji wa leseni kwa wavuvi waliokidhi viwango. Aidha, leseni kwa wavuvi watanzania zitolewe kwa kutumia shilingi ya Tanzania na siyo dola ya kimarekani kama ilivyo sasa.Hii itaongeza tija ya matumizi ya fedha yetu.
ii. Serikali ichukue jukumu la kuelimisha wavuvi juu ya sheria za uvuvi na uhifadhi wa mazingira pia kukuza ujuzi wa wavuvi wadogo kwa kuwapatia mbinu nzuri za uvuvi,matumizi sahihi ya nyenzo za Uvuvi,kuongeza uelewa kwa wavuvi kuhusu tabia za bahari na namna ya kutumia tabia hizo za bahari pia kuweka utaratibu mzuri wa kusajili yombo vyao vya Uvuvi.
iii. Serikali iweke mazingira wezeshi kwa wavuvi kupata zana bora za uvuvi na kwa bei nafuu ili kusaidia uvuvi salama na endelevu kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
iv. Serikali iweke mpango madhubuti wa kudhibiti uvuvi wa kina katika bahari (deep sea fishing) kwa kutoruhusu wangeni kukwepa kodi.
v. Serikali inunue mashine zenye teknolojia ya kuweza kuwabaini wezi wa kigeni wa mazao ya baharini na kutoa mafunzo kwa wataalam wazawa ili waweze kudhibiti uvuvi katika bahari kuu.
5. MIRADI YA KITAIFA YA KIMKAKATI
5.1. Miundombinu ya Reli
Mheshimiwa Spika, wakati mataifa yaliyoendelea duniani yanawekeza katika miundombinu ya reli ambayo inachangia sana ukuaji wa uchumi, Tanzania tumeendelea kukumbatia usafirishaji kwa njia ya barabara ambapo uchangiaji wake katika ukuaji wa uchumi ni mdogo uklinganisha na ule wa reli. Hata hivyo miundombinu ya barabara imekuwa ikiharibika mara kwa mara kwa sababu ya kuzidiwa na mizigo ambayo ingeweza kusafirishwa kwa njia ya reli kama Serikali ingewekeza vya kutosha kwenye reli. Aidha, usafiri kwa njia ya barabara umekuwa chimbuko la ajali nyingi ambazo zimeondoa uhai wa wananchi wengi na hivyo kuendelea kupunguza nguvu kazi ya taifa.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na Serikali kuanisha miundombinu ya Reli kama mojawapo ya miradi ya Kimkakati, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni kama serikali iko “serious” na ujenzi wa reli nchini. Hii ni kwa sababau huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mika mitano, lakini Mpango unaonyesha kwamba ujenzi wa reli uko katika hatua za mwanzo kabisa za utekelezaji. Kwa mfano, Ukarabati wa Reli (Kaliua – Mpanda) zimetengwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kufanya usanifu kwa ajili ya ujenzi wa stesheni na ghala la mizigo Mpanda. Aidha, Mradi wa Reli ya Kati ya Tabora – Kigoma na Isaka – Mwanza, zimetengwa jumla ya shilingi bilioni 11.7 kwa ajili ya usanifu wa kina wa njia ya reli kwa kiwango cha kimataifa “standard gauge” kati ya Tabora- Kigoma na Kaliua – Mpanda, kukamilisha kazi ya usanifu wa kina wa njia ya reli kwa kiwango cha kimatafa kati ya Isaka – Mwanza; Upembuzi yakinifu wa mradi kwa ajili ya njia mpya ya reli kati ya Uvinza – Msongati na Mpanda – Karema, na ununuzi wa eneo kati ya Mpanda – Karema kwa ajili ya njia mpya ya ya ukanda wa Mpanda – Karema.
Mheshimiwa Spika, Ujenzi na uboreshaji wa reli (DSM-Isaka- Kigali) zimetengwa shilingi milioni 500 kwa jaili ya upembuzi wa kina, mradi wa reli Mtwara – Mbamba Bay na Mchuchuma - Liganga umetengewa shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa; Mradi wa Reli Tanga – Arusha – Musoma nao umetengewa shilingi bilioni 9.1 kwa ajili ya usanifu wa kina na michoro kati ya Tanga – Arusha, na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kati ya Arusha – Musoma. Aidha, mradi wa usafiri wa treni Daresalaam umetengewa shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa awali wa njia mpya za reli Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi karibu yote ya ujenzi wa reli, iko katika hatua za awali za utekelezaji licha ya kwamba huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Fedha takriban zote zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa reli ni kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, kufanya usanifu, kufanya tathmini, kufanya usanifu wa kina nk. ukiwa ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango. Hii ina maana kwamba fedha iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya reli itatumika kuwalipa washauri waelekezi na wasanifu mishahara na posho badala ya kutumika kununulia vifaa vya ujenzi halisi wa miundombinu ya reli moja kwa moja. Kwa maana nyingine, fedha za miradi ya maendeleo zinatumika kama matumizi ya kawaida, ndio maana miaka mitano ya Mpango wa Maendeleoa inamalizika, hakuna reli iliyojengwa.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali hii ya CCM imeamua kutumia kichaka cha miradi ya maendeleo kukwapua fedha za maendeleo na kuanza kuzitumia kama matumizi ya kawaida kwa kulipana posho na mishahara, na kwa kuwa kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa Serikali imeshindwa kututekeleza mpango huo kwa ufanisi; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuwatangazia wananchi wote kwamba; malengo ya dira ya taifa ya 2025 hayawezi kufikiwa kama CCM itaendelea kutawala.
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kama miaka mitano imetumika kufanya upembuzi yakinifu, bila shaka miaka mingine mitano itakuwa ni kutafuta washauri waelekezi, halafu miaka mingine mitano itatumika kutafuta wazabuni na kwa maana hiyo mwaka 2025 utafika bila ujenzi rasmi wa reli kuanza. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuwataarifu wananchi wote kwamba, ikiwa wanapenda kweli kuona maendeleo katika sekta mbalimbali yakitokea, basi waiondoshe Serikali ya CCM amabyo kwa miaka yote 53 ya Uhuru bado iko kwenye upembuzi yakinifu na kuiweka Serikali Mpya inayotokana na UKAWA, ili itimize ndoto za muda mrefu za wananchi za kuondokana na umasikini uliokithiri na adha mbalimbali za maisha kutokana na miundombinu duni.
5.2. Miundo Mbinu ya Barabara
Mheshimiwa Spika, Pamoja na miradi mingi ya barabara kuwa chini ya kiwango na licha ya miradi mingine kuwa katika ahadi tu bila utekelezaji kwa mfano mradi wa barabara za juu (fly overs) katika jiji la Dar es Salaam, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kujikita zaidi katika Mradi wa Mabasi yaendayo kasi – DART.
Mheshimiwa Spika, mradi wa DART unajengwa kwa wigo finyu kana kwamba utatumika kwa miaka mitano au kumi tu. Nasema hivi kwa sababu mradi huu unajengwa katika barabara kuu zinazongia katika kitovu cha Jiji la Dar es Salaam na kwa maana hiyo wigo wake ulitakiwa kuwa mpana ili kuondoa tatizo la msongamano wa magari ambalo limekuwa tatizo sugu la Jiji la Dar es Salaam kwa sasa. Aidha, mradi huu uko katika barabara ya Morogoro ambayo inaunganisha nchi yetu na nchi jirani, hivyo mradi huo ulitakiwa kuwa kioo cha nchi yetu kwa wageni wanaoingia nchini mwetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitegemea upanuzi wa barabara ile ungeendana na mahitaji ya kisasa ili kutatua tatizo la foleni lakini pia kuwa na ubora wa hali ya juu ili mradi huo udumu na kusaidia vizazi vijavyo. Lakini kinyume chake Barabara za Mradi wa DART zina mapungufu makubwa ikiwemo barabara zake (lanes) kuwa nyembamba sana na hivyo kuwa chanzo cha ajali hasa maeneo ya Kimara Matangini. Adha, kumekuwa na matuta kila baada ya mita chache jambo ambalo linaondoa dhana ya kuwa barabara kuu (highway).
Mheshimiwa Spika, Wembamba wa barabara hiyo ya mradi wa DART unatokana na Serikali kutozingatia Master Plan ya Jiji la Dar es Salaam. Ushahidi wa hili ni makazi mengi kuwa kwenye hifadhi ya barabara lakini pamoja na hayo bado wananchi wengi wana hati za umiliki wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni kwanini imetoa hati ya umiliki wa ardhi katika maeneo ya hifadhi ya barabara na kuwaacha wamiliki hao kujenga nyumba katika hifadhi ya barabara, na wakati huohuo kuwafukuza na kuwachukulia bidhaa zao wafanya biashara ndogondogo wanaotafuta riziki yao ya siku pembezoni mwa barabara? Kwanini Serikali inakuwa na double standard katika kushughulikia tatizo la uvamizi wa hifadhi za barabara kama inafuata sheria? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kujifunza kutoka katika barabara ya Thika Super - Highway Jijini Nairobi – Kenya ambayo ina upana wa kutosha kuchukua hadi mistari nane ya magari na hivyo kuondoa kero ya foleni.
6. VIWANJA VYA NDEGE
Mheshimiwa Spika, Ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege unaendelea kwa kusuasua sana. Mfano mzuri ni upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Serikali imekuwa ikitoa kauli mara kwa mara kuhusu kukamilisha ujenzi huu, lakini ujenzi huo unakwenda kwa kasi ndogo sana jambo linaloashiria kwamba pengine Serikali haimlipi Mkandarasi kwa wakati ndio maana ujenzi unasuasua. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuongeza kasi ya ujenzi huo ambao umekuwa ukichukua muda mrefu jambo ambalo linasababisha huduma za usafiri kuwa duni lakini pia gharama za ujenzi huo kuendelea kuongezeka kutokana na shilingi yetu kuendelea kuporomoka.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, hivi karibuni kuliibuka kashfa ufisadi katika ujenzi wa eneo la wageni mashuhuri (VIP Lounge) katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, tuhuma ambazo zimewahi kuwasilishwa katika Bunge lako tukufu na Kamati ya PAC. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza imechukua hatua gani juu ya ufisadi huo Kama ilivyoripotiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa mwaka uliopita?
7. UPIMAJI NA UPANGAJI WA MATUMIZI YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa tumeshuhudia migogoro mikubwa ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Migogoro hii mara kwa mara imesababisha mauaji ya watu wengi.
Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo yamekumbwa na migogoro ya wakulima na wafugaji ni pamoja na Mvomero, Kilosa Mkoani Morogoro, Rufiji, Chalinze Mkoani Pwani. Moja ya suluhisho la jambo hili ni pamoja na kupima ardhi nchi nzima pamoja na kugawanya maeneo ya ardhi ya wakulima na wafugaji. Kambi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kupima ardhi yote nchini na kuigawa kulingana na matumizi mbalimbali, lakini Serikali haijawahi kuufanyia kazi ushauri huu. Kwa kuwa Serikali haijatekeleza usharui tulioipa, migogoro ya ardhi imekuwa ikiendelea kila kukicha na hivyo kuendela kusababisha hali ya utulivu na amani miongoni mwa jamii kutoweka. Kwa kuwa Serikali imepuuzia jambo hili, Serikali mpya ya UKAWA itaweka suala la upimaji ardhi na kuigawa katika matumizi mbalimbali kwenye vipaumbele vya majukumu ya Serikali.
8. UGHARAMIAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2011/12 – 2015/16 ulikadiriwa kugharimu shilingi trilioni 8.9 kila mwaka ambapo shilingi trilioni 2.9 zilitakiwa kutokana na fedha za ndani katika bajeti ya Serikali na shilingi trilioni 6 zilitakiwa kutokana na uwekezaji wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizo tu inaonyesha kwamba taifa linagharamia Mpango wake wa Maendeleo kwa asilimia 32.5 tu. Asilimia 67.5 ya gharama za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa zinategemewa kutokana na misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo ambayo haina uhakika wa kutolewa kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, licha ya tengeo dogo la fedha za ndani kugharamia mpango, bado fedha hizo hazitolewi kwa wakati jambo ambalo linakwamisha miradi mingi ya maendeleo. Kwa mfano mapitio ya ugharamiaji wa Mpango mwaka 2014/15 yanaonyesha kwamba ni asilimia 39 tu ya bajeti ya maendeleo iliyokuwa imetolewa na Serikali hadi kufikia Machi, 2015. Hata hivyo, hakuna uhakika kama asilimia 61 ya bajeti ya maendeleo iliyobaki inaweza kutolewa kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kugharamia Mpango wa Maendeleo kwa fedha za ndani angalau kwa asilimia 50 kuliko ilivyo sasa ambapo inagharamia asilimia 32.5 tu. Athari za kuacha asilimia kubwa ya ugharamiaji wa Mpango itolewe na wahisani, miradi ya maendeleo haitekelezwi hasa ukizingatia kwamba wengi wa wafadhili wamesitisha misaada ya maendeleo kutokana na kukithiri kwa rushwa na ufisadi Serikalini.
9. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, hotuba yangu nimeeleza jinsi ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali hii ya CCM juu ya utekelezaji bora wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa lakini Serikali imeendelea kuwa na shingo ngumu kutekeleza mapendekezo tuliyoipatia. Aidha, nimeonyesha jinsi ambavyo Serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza ilani yake ya uchaguzi kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, Nimeeleza pia jinsi ambavyo miradi ya maendeleoa inavyotekelezwa kwa kususua. Hoja hii imetokana na uhalisia kwamba huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano lakini miradi mingi iko katika hatua za awali za utekelezaji. Hii ina maana kwamba fedha nyingi za maendeleo katika hatua hii, zinatumika kama matumizi ya kawaida ya uendeshaji kwa maana ya kuwalipa wasanifu, wapembuzi yakinifu mishahara na posho badala ya fedha hizo kutekeleza miradi hiyo moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshauri Serikali kugharamia Mpango wa Maendeleo angalau kwa asilimia 50 ili nchi isikwame ikiwa wahisani na washirika wa maendeleo watagoma kama ilivyo sasa kutokana na ufisadi serikalini.
Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuwaambia wananchi kwamba Serikali hii ya CCM haina nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo. Hii ni kwa sababu kwa miaka yote imekuwa ikitenga bajeti ndogo ya maendeleo katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Licha ya kutenga bajeti ndogo ya maendeleo, bado fedha hiyo pia imekuwa haitolewi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM imekuwa hodari sana kujitetea inaposhindwa kutekeleza miradi yamaendeleo kwa kutoa kisingizio kwamba wahisani wajatoa fedha. Lakini pia inafahamu ni kwa nini wahisani hawatoi fedha. Ni kwa sababu ya rushwa!!!!
Mheshimiwa Spika, CCM yenyewe inakiri katika chapisho lake la Mwelekeo wa Sera za CCM 2000-2010 ukurasa wa tatu kwamba wahisani hawatoi fedha kutokana na rushwa na ufisadi serikalini. Chapisho hilo linasomeka hivi: “Mwaka 1994 na 1995 wahisani walisimamisha misaada kutokana na rushwa, hivyo kupelekea uchumi wa nchi kuyumba” mwisho wa kunukuu. Kumbe hii si mara ya kwanza wahisani kusimamisha misaada, na CCM wana uzoefu na jambo hili.
Mheshimiwa Spika, kutoka mwaka 1994 mpaka leo, ni zaidi ya miaka 20 jambo lilelile la ufisadi na rushwa, katika serikali ya Chama kilekile linaendelea kututafuna kama Taifa. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka wananchi wote watambue kwamba kuendelea kuwa na CCM madarakani ni janga la Taifa. Hii ni kwa sababu tutaendelea kutoaminiwa na jumuiya ya kimataifa na hivyo kuendelea kukosa misaada ya kibajeti na watakaothirika ni wananchi wanyonge ambao ni wanufaika wakuu na misaada hiyo katika huduma za afya, elimu, miundombinu nk. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa wito kwa wananchi wote kuchagua viongozi wanaotokana na UKAWA katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015 ili tupate Serikali mpya inayotokana na vyama vya Upinzani na kurejesha tena imani yetu mbele ya jumuiya ya Kimataifa ambayo ilishapotea kutokana na ufisadi wa CCM. Aidha, Serikali mpya ya UKAWA, itahakikisha kwamba inagharamia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa asilimia 50 ili kupunguza utegemezi kwa wahisani katika bajeti ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nawatakia wabunge wote kila la heri katika maisha yao watakapokuwa uraiani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Esther Nicholas Matiko (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA NCHI OFISI YA RAIS – MAHUSIANO NA URATIBU
15 Juni, 2015
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA NCHI OFISI YA RAIS – MAHUSIANO NA URATIBU
15 Juni, 2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni