
Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu
mkoani Kigoma, imeelemewa baada ya idadi ya wakimbizi kutoka Burundi
kuzidi kuongezeka hivyo kuzidi uwezo wake kama inavyotakiwa na sheria za
Umoja wa Mataifa (UN).
Mkurugenzi Idara ya Wakimbizi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke,
alisema bado wakimbizi wa Burundi hawajaanza kurudi nyumbani kwao bali
hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na idadi yao kuendelea kuongozeka.
Kwa mujibu wa Mseke, hadi sasa wakimbizi
katika kambi hiyo kutoka Burundi, wamefikia 71,000 na ndani ya wiki
moja iliyopita wameingia wakimbizi 10,000.
Alisema kwa sasa idadi ya wakimbizi wote kutoka Burundi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), katika kambi hiyo ni takribani 100,000.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, idadi
hiyo ni kubwa kupita kiasi kwani sheria za UN kupitia shirika lake la
kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) kambi moja inapaswa kuhudumia wakimbizi wasiozidi 50,000.
“Kuna
tatizo kubwa la eneo la kuwaweka kwani wakimbizi wote kutoka Burundi na
DRC, bado wanahifadhiwa katika kambi ya Nyarugusu. Kwa sheria za
Umoja wa Mataifa, kambi moja inatakiwa kuwa na wakimbizi 50,000, lakini
sasa wapo zaidi ya 100,000.
Mseke, alisema hadi sasa serikali
inafanya utaratibu wa kujenga kambi nyingine ili kupunguza idadi hiyo na
kuangalia uwezekano wa kuwatenganisha wakimbizi hao kutoka nchi hizo.
Ongezeko la wakimbizi kutoka Burundi,
limechangiwa na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo baada ya
Rais wake, Pierre Nkurunzinza, kutangaza kuwania urais kwa kipindi
kingine cha tatu hivyo kudaiwa kukiuka katiba ya taifa hilo.
SOURCE:Nipashe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni