kitu ambacho kila binadamu anakipitia kabla ya kuzeeka basi ni utoto. Pamoja na mambo mengine kila mtu hata Rais wetu amewahi kuwa mtoto hivyo si ajabu kusema kwamba licha ya sasa kupigiwa salute na mizinga 21 lakini ukweli unabaki pale pale kwamba aidha amewahi kuchezea matope au kuramba kamasi yake. Hata wachungaji wakubwa na maimamu wanaoswalisha huko makanisani na misikitini huwezi amini kwamba kuna kipindi walikuwa hawawezi kula bali walikuwa wanalishwa na wazazi wao.
Ndiyo, hiyo ni hatua ya utoto na hayo ndiyo badhi ya mambo ya kitoto. Kawaida ya mambo ya kitoto ni kwamba huwa yanapita na hayajirudii tena kwa namna, hali na sifa ile ile. Na kila mmoja analo tukio ambalo kamwe hawezi kulisahau toka enzi za utoto wake mpaka leo.
Sasa nami pia kuna tukio la kimichezo ambalo lilifanyika mwaka 2001 katika kata ya Ijoka huko jimboni Rungwe Masharikiki katika kijiji cha Mpombo two (2). Sisi vijana tuliotoka Mpombo One tulikwenda kushindana ugenini na kama kuna kitu tulienda nacho basi ni mpira mmoja tu ule wa karatasi za nailoni kwa kule kwetu tunaita 'Kiniengo'. Lakini vingine vyote tulivikuta kule akiwemo Refa, Kamisaa na mashabiki.
Basi ilipofika saa kumi tulianza kabumbu pale shule ya msingi Lusanje, awali ilionekana kama mechi nzuri na ingekuwa ya haki lakini kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda hali ilibadilika. Ieleweke kwamba hakukuwa na muda maalumu wa mapumziko hivyo lilikuwa ni suala la kukubaliana kwamba baada ya timu kufungwa goli mbili basi ni "half time". Mimi binafsi nilikuwa natamani muda wa kubadilishana magoli ufike maana Mpombo Two Sports Club walikuwa wakipeleka mpira upande wa kaskazini hivyo walikuwa wanasaidiwa na upepo.
Sasa mazingira ya shaka yalizidi baada ya sisi Mpombo One Sports Club kufunga goli zuri la kichwa, nakumbuka goli hilo lilifungwa na Andambike Mwalunyasyo (Mungu amlaze pahala pema peponi), baada ya kuwafunga refa aliyejulikana kwa jina moja la A.K.A Mwakaleli aliamuru eti siye tuliofunga tuvue tisheti zetu badala ya waliofungwa ili tueleweke naye apate kututofautisha kwa kuwa hatukuwa na jezi. Mimi nilijaribu kubisha kwa kuwa ilikuwa kinyume cha utaratibu wa kawaida badala yake alipuliza kipyenga chake na kuniita, aliniambia niiname kisha akanikong'oli kichwani.
Baada ya mabishano tukakubali tuvue mashati licha ya kutangulia kuwafunga. Mpira uliendelea na gafla pasi ndefu ikapigwa na kumkuta Job Mwakalinga nambari 11 naye hakufanya ajizi akafumua shuti kali lililomshinda golikipa wao. Cha kushangaza refa alilikataa akidai kwamba mfungaji aliupiga vibaya mpira kwani alitumia vidole kupiga mpira, aling'aka "ukomiile inyobhe". Mashabiki wakaunga mkono uamuzi wa refa pamoja na kamisaa.
Hatukuwa na namna maana uwanja ulikuwa wao, mashabiki ni wao, refa ni wa kwao, kamisaa ni wa kwao na mpira tuliokuwa tunaucheza ulikuwa wa kwao...sasa tungefanya nini?
Tulipoona hali ni tete mpaka saa kumi na mbili toka saa kumi jioni bila mapumziko, tuliomba 'half time' ili na sisi tuelekeze mpira upande wa kaskazini walau nasi tusaidiwe na upepo lakini refa aligoma akidai hatukuwa na haki hiyo, wenye haki ya kulalamika walikuwa wale waliofungwa na siyo sisi. Mimi nilikuwa nimechoka kweli na hapo nikiwa goli kipa, nikamnong'oneza rafiki yangu Lwitiko kwamba tupaki basi yaani wote warudi nyuma na wakafanya hivyo. Cha ajabu refa akasimamisha mpira akidai huo si mchezo hivyo tusambaratike ili mechi iendelee.

Kwa kuwa tulikuwa tumechoka kuonewa mimi nikasema hakuna kitu kama hicho, wenzake wakaniunga mkono. Basi kwa hasira Refa aliamuru wachezaji wa Mpombo Two wenye viatu wavae kinyume na makubaliano yetu ya awali kwamba wote tucheze peku peku ili tusiumizane.
Kwa kuwa mpaka wakati huo ilikuwa karibia saa 18:30, na sisi tuliamua kuvaa tisheti zetu ili tusiwe matumbo wazi kwakuwa baridi ilianza kuwa kali. Tulimwomba refa amalize mechi maana tulikuwa tumecheza kama saa la tatu mpaka hapo, refa alikuwa mkaidi akidai hadi ifike saa moja. Basi kwa ishara zetu tukapashana habari , baada ya kufanya mashambulizi ya kushitukiza ulipigwa mpira mbali kabisa na wakati wanahangaika mashabiki wao kuokota mpira siye tukatoka uwanjani na kuanza kukimbia kurudi nyumbani. Refa alitutukana na kutudharau lakini hatukujali.
Hayo ndiyo yanayowakumba Mhe.John Mnyika na Mnadhimu mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Mhe.Tundu Antipas Lissu mbele ya refa wa bungeni Mhe.Spika Anne Makinda. Mfano jana Mhe.Makinda akadai hakuna wa kumlazimisha afanye nini na hiyo ilikuwa ni baada ya Mhe.Mnyika kuomba mwongozo wa kiti baada ya miswada minne ambayo ni muswada wa Sheria ya Kulinda watoa taarifa za uharifu; muswada wa sheria ya Petroli; muswada wa sheria ya usimamizi wa mapitio ya mafuta na gesi na muswada wa Sheria ya uwazi na uwajibikaji katika tasinia ya uchimbaji wa mwaka 2015.
![]() |
Mhe.Mnyika na Tundu Lissu |
Wapinzani wanasema miswada hii imeletwa kwa hati ya dharura ili kuwaburuza wabunge na kupitisha mambo yasiyokuwa na maslahi kwa umma.
Kwa msimamo huo wa wapinzani mathalani Mhe.Mnyika refa wa bungeni Mhe.Makinda anawaona wanakiuka taratibu. Wanamtajia vifungu vya kanuni anavyokiuka lakini bado tu anataka watulie. Kiufupi ni kwamba hakuna haja ya kuharakisha mambo yenye maslahi ya muda mrefu kwa umma, mfano muswada pekee wa mafuta na gesi una vifungu 261 na vifungu vidogo zaidi ya 3000 kwanini ijadiliwe kwa haraka haraka tena kwa hati ya dharura?
Kwa mwendo huu ni bora Mhe.Mnyika, Tundu Lissu na wana UKAWA kwa ujumla wawaite wapenda vurugu bungeni ila endeleeni kusimamia haki licha ya kwamba mnacheza mechi ya ugenini, kamisaa ni wao, refa ni wao na mpira ni wao.Fungeni goli la mapema harafu wote mrudi nyuma maana dakika ni za majeruhi na refa aitwao Mwakaleli hataki haki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni